In Summary
  • Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ndiyo waendeshaji wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka katika nchi tofauti anapopatikana mdhamini.

Michuano ya Kombe la Chalenji inatarajiwa kuanza Novemba 24 hadi Desemba 6 nchini Kenya.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ndiyo waendeshaji wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka katika nchi tofauti anapopatikana mdhamini.

Michuano hiyo itafanyika baada ya kupita miaka miwili bila kuchezwa na Tanzania imethibitisha kupeleka timu zake zote za wanaume na wanawake.

Pia Tanzania imethibitisha kushiriki Kombe la Chalenji kwa timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika Bujumbura, Burundi kuanzia Desemba 12 hadi 22.

Mbali na Tanzania Bara, pia zimo Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia. Zimbabwe na Libya ni waalikwa.

Tanzania Bara itawakilishwa na timu ya ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’. Mara ya mwisho Kilimanjaro Stars ilitwaa Kombe la Chalenji mwaka 2010 baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa makubaliano, timu zote zitakazoshiriki Kombe la Chalenji zinatakiwa kupeleka kikosi cha kwanza lengo ni kuhakikisha kunakuwepo ushindani na kukuza kiwango cha soka cha Afrika Mashariki na Kati.

Tarehe rasmi ya kuanza michuano hiyo imetangazwa, hivyo ni jukumu la Tanzania kujiandaa vyema kushindana na hatimaye kutwaa ubingwa.

Timu za taifa zinatakiwa kuanza maandalizi mapema ili kuwajengea wachezaji uwezo wa kufanya vyema katika mechi zao.

Hakuna njia ya mkato kwa timu kupata mafanikio kama haitafanya maandalizi ya kutosha kuwajengea uwezo wa kucheza mechi zao kikamilifu na ikiwezekana kuleta kombe Tanzania. Watanzania wana kiu ya ubingwa kwa kuwa kwa muda sasa hawajawahi kuzipokea timu kwa shangwe.

Tumekuwa na tabia ya kuteua wachezaji wenye maumbile madogo, lakini wenye umri mkubwa na kuwaweka kwenye timu zetu za vijana. Huku ni kutafuta mafanikio kwa kujidanganya.

Ni bora kuwa na timu ambayo haitafanya vizuri kwenye mashindano hayo, lakini yenye wachezaji wenye umri sahihi ambao watalifaa Taifa hapo baadaye watakapokuwa tayari.

Ni muhimu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha linapata wachezaji wenye umri sahihi ambao wataandaliwa kwa muda wa kutosha ili wafanye vizuri kwenye mashindano hayo na baadaye walisaidie Taifa wakati watakapofikia kiwango hicho.

Suala hilo pia ni muhimu kwa timu ya wanawake itakayoshiriki mashindano hayo. Ligi ya wanawake ni kubwa ambayo haiwezi kutoa picha halisi ya kiwango chetu cha soka. Ni kweli kwamba tumechelewa, lakini Chalenji inafaa kutuamsha kuwa tunatakiwa tuwe na mashindano sahihi yatakayotuwezesha kupata timu nzuri ya Taifa.

TFF pia inatakiwa isuke mkakati wa jinsi ya kuyatumia mashindano ya Cecafa ambayo yamefufuliwa. Je, ni mashindano ambayo yatatulazimisha kuwaita akina Mbwana Samatta na wengine walioko barani Ulaya au kujaribu wachezaji wa ndani?

Ni muhimu TFF ikawa na sera hiyo ambayo itamsaidia kocha kuandaa timu kulingana na malengo ya shirikisho. Ili timu ya Taifa iwe nzuri, kocha anatakiwa ajaribu wachezaji wengi kadri awezavyo na atafanikisha hilo akiwa na mashindano mengi.