In Summary
  • Changamoto hii inawakumba kwa sababu staili ya maisha haiwapi fursa ya kujifunza kufikiri. Kila kitu kinafanywa kama siyo na msaidizi wa nyumbani, basi itakuwa mashine au namna yoyote ya utandawazi.

Moja ya changamoto kubwa zinazowakumba vijana ni uwezo wa kukabiliana na maisha, ikiwa ni pamoja na majukumu, uwezo wa kufikiri na kupata majibu ya matatizo yao na kutatua shida mbalimbali za jamii wanayoishi.

Changamoto hii inawakumba kwa sababu staili ya maisha haiwapi fursa ya kujifunza kufikiri. Kila kitu kinafanywa kama siyo na msaidizi wa nyumbani, basi itakuwa mashine au namna yoyote ya utandawazi.

Muda ambao kijana angejifunza kujitegemea kwa kufanya kazi anaumaliza katika mtandao au soga katika makundi sogozi ambayo hayamwongezei uwezo wa kufikiri bali kujifunza mambo ambayo hayaendani na umri wake wakati mwingine.

Unaweza usilione tatizo hili kama si mfuatiliaji mzuri wa maswala ya kijamii, lakini lipo miongoni mwa vijana wadogo wanaoelekea kujitegemea, uwezo wa kujituma katika majukumu yao, kuchanganua mambo hususani yanayowahusu maisha, umekuwa mdogo sana kiasi ya kwamba ninaanza kuziona familia zijazo zikiwa legevu au zikikosa kuwa na wazazi wanaoweza kutatua changamoto za familia zao.

Hili sio jambo ambalo limeibuka kusikojulikana, la hasha, kuna chanzo na kama tutashindwa kurekebisha kwa sasa kuna hatari kubwa miaka inavyozidi kwenda tukajenga jamii ya vijana wasioweza kujitegemea, wavivu, wasioweza kukabili majukumu yao katika familia na jamii zao.

Kijana ambaye anafanyiwa kila kitu huenda akashindwa kuiongoza nyumba yake au ofisi atakapokabidhiwa. Hajui kukabiliana na majukumu kwani amekuwa akifanyiwa kila kitu.

Kwa wale ambao tumekulia vijijini watakubaliana na mimi kuwa vijana waliokuwa katika familia za kipindi cha nyuma kuna elimu ya jamii walikuwa wanaipata katika familia zao hususani ya kujitegemea, kufanya kazi, kujituma, kutambua majukumu yao jambo ambalo lilifanya vijana wale kuwa jasiri, wenye uwezo wa kufikiri huku ikiwaandaa kuwa baba na mama wazuri katika familia zao tofauti na sasa.

Upande wa majukumu katika familia ukweli ni kuwa miaka ya nyuma vijana walijifunza kujitegemea katika maswala yanayowahusu na walipewa majukumu katika familia.

Masuala kama kufua nguo zako, kuosha vyombo ambavyo umevitumia, kufanya usafi katika nyumba, pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo za nyumbani zinazoendana na umri wako.

Haya hayakuwa majukumu ya msichana au mfanyakazi wa ndani, yalikuwa ni majukumu ya watoto wa familia kwa ujumla na kila mtoto alikuwa akitambua jukumu lake pindi afikapo nyumbani akitokea shuleni.

Majukumu hayo kwa sasa husuani katika maeneo ya mjini yamebadilika na sasa ni ya msichana wa kazi kuhakikisha kuwa nguo za mtoto (hata kama ana miaka 16) zimefuliwa, nyumba imefanyiwa usafi na vijana wapo wamepumzika na majukumu mengine huku tukiamini mtoto kazi yake ni kusoma elimu ya darasani ili afaulu tu.

Naungana na wanaosema kuwa mazingira yamebadilika na dunia imebadilika kwamba majukumu ya familia nayo yamebadilika kutokana na ujio wa utandawazi na teknologia. Ni kweli wengine wanaenda mbali Zaidi na kusema sio lazima vijana wa sasa kulelewa kama ilivyokuwa zamani, lakini kuna mambo lazima tukubali kuwa mtoto anapaswa kuyamudu kuyafanya mwenyewe akiwa nyumbani maana hatujui kesho ataishi wapi na atakuwa nani.

Hivi ni kweli mtoto hana haja ya kufahamu kufanya usafi wa nyumba anayoishi? Mtoto hahitaji kufundishwa kufua nguo zake mwenyewe? Mtoto hahitaji kufahamu kuosha sahani yake aliyoitumia kula chakula? Nadhani maswala madogo madogo kama haya yatupasa kuwaelekeza watoto wetu wakiwa wanakuwa na inawajengea uwezo wa kujituma na kuweza kuchangamsha akili zao katika kufanya kazi.

Tumekuwa tukilalamika kuwa vijana wengi hawapendi kufanya kazi, wavivu, wanaishia kutumia vilevi na madawa ya kulevya, haya yote ni matokeo ya malezi ya kuwadekeza watoto wetu tukiamini kuwa kuwapa kazi ndogo ndogo nyumbani ni kuwaonea au hawastahili kupewa kazi kabisa.

Ni lazima sasa wazazi turudi nyuma na kufikiri ni wapi tulikosea katika hili ili tulirekebishe kwa haraka na kurudi katika mstari uliosahihi ili kuweza kuwatengeneza watoto wetu waje kuwa wazazi bora wanaoweza kujituma na kufanya kazi bila uvivu katika miaka yao baadaye.

Ufanyaji kazi za nyumbani husaidia kuchangamsha akili ya kijana na kumwongezea uwezo wa kufikiri. Kwa mfano anapokuwa na ulazima wa kuifanya kazi fulani kila siku, lazima atatafakari namna rahisi ya kuifanya kazi hiyo.

Si hivyo tu, kazi humsaidia mtoto kujifunza kupanga ratiba zake. Kijana anapotaka kufanya maongezi na wenzake, au kujisomea lazima atahakikisha kazi zake haziharibu mpango wake.

Exaud Mtei

0712098645/0752402602