In Summary
  • Mkutano ule haukuiacha salama Zanzibar. Ilifutiwa uanachama wake iliyodumu nao kwa siku 128 baada ya kuandikwa kuwa mwanachama wa 55 wa CAF.

Mkutano wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, uliofanyika kule Rabat nchini Morocco, ulikuja na maazimio mengi kwa soka la Afrika.

Mkutano ule haukuiacha salama Zanzibar. Ilifutiwa uanachama wake iliyodumu nao kwa siku 128 baada ya kuandikwa kuwa mwanachama wa 55 wa CAF.

Masikini Zanzibar kumbe uanachama wake uliandikwa kwa kalamu ya risasi ambayo ukichukua kifutio kwa wale wanaokumbuka shule ya msingi, ikafutwa mara moja na sasa si mwanachama.

Zanzibar walisikitika na Watanzania kwa jumla, lakini hilo sasa linabakia historia. Linabakia hivyo kuwa Zanzibar si mwanachama tena na kinachotakiwa ni kusonga mbele.

Kuna mengi yalianzishwa kwa mgongo wa CAF.

Kuunda mfumo wa Ligi Kuu, kutengeneza timu za Ligi kuu na mifumo mbalimbali ya soka kwa Zanzibar, sasa hayo yaendelezwe bila kujali kuwa CAF imevunja mwiko.

Ni mipango mizuri kwa maendeleo ya soka Zanzibar. Ni sawa na msiba, unapotokea ni kumshukuru Mungu na maisha lazima yaendelee.

Zanzibar kuendelea kusononeka haitawasaidia. Niliwahi pia kuandika haya. Ijipange maisha yasonge kwa sababu hilo la uanachama halipo tena.

Lengo si kuingia huko, mada yangu ya leo ni kuangalia mabadiliko ya CAF hasa kwa timu za taifa kuongezwa kutoka 16 hadi 24.

Mkutano ule wa CAF ambao tulielezwa kuwa Makamu wa TFF, Wallace Karia alihudhuria, pamoja na misukosuko yake, niliwaza tu kuwa baada ya kurejea kutoka Morocco, angewaita wadau wa mpira, wachezaji wa zamani, makocha na kuwapa mrejesho na kisha kutengeneza mkakati ya 2019.

Inawezekana CAF wakaja na muundo wa nyongeza ya mashindano japokuwa haijaliweka sawia, lakini hakuna hata kilichoelezwa kutoka Morocco.

Tanzania ilicheza mechi moja na Lesotho na kutoka 1-1, nini maandalizi yanayofuata. Msingi lazima ujengwe sasa ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa mataifa manane yatakayofaidi nyongeza ya timu nane za fainali za Afcon 2019.

Tumeshindwa kwa miaka inayofikia 40. Tulicheza Fainali za Afrika 1980 timu zikiwa nane, timu zimeongezwa kutoka nane hadi 16 nayo tumehangaika kufuzu na sasa zimeongezeka kutoka 16 hadi 24, nayo tutashindwa kweli!

Ingeundwa kamati ya kuhakikisha Stars inasonga mbele, inakwenda Cameroon 2019 kwa vitendo. Kamati ikae, ichague wanasoka wa kuipeleka Stars Cameroon lakini si kukaa mezani na kusema ‘Road to Cameroon 2019’, kusema hayo ni rahisi, tuje kwenye vitendo.

Kamati iwe nje ya wanaowania uongozi TFF, na watakaoingia wawe na mwendelezo wa Taifa Stars kwamba tayari kuna msingi.

Ninafahamu kila anayekuja kwenye utawala anakuwa na mambo na watu wake, huu uwe msingi imara usiofungamana na upande wowote na watakaoingia TFF, waendeleze watakapowakuta.

Waganda walidhamiria, walikaa wakajipanga na mwaka huu wamekwenda Fainali za Gabon tena wao mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1978.

Pamoja na kufanya vibaya Fainali za Afcon za Gabon, wameonyesha kunogewa, wamepania kurudi Cameroon 2019 huku wakiwatumia wachezaji wanaocheza nje.

Tusidanganyane, kama mikakati haikufanyika sasa, Fainali za Afcon 2019 tutazisikia kwenye bomba na kuongeza wigo wa miaka ya kuzikosa ilhali wigo wa timu umeongezeka.

Kingine ambacho hatukioni japokuwa kipo, uzoefu unaonyesha hakuna taifa lililofuzu AFCON kwa wachezaji wa ligi za ndani, labda iwe kama Misri lakini asilimia kubwa ni wachezaji wanaocheza nje.

Huwa ninajiulizaz, nini kinakwamisha kuwapata wachezaji wetu wa nje?

Hata kama hatuwafahamu, wachezaji waitwe na tuwaone. Mbona wapo!

Dk Mshindo Msolla akiwa kocha wa Stars alimuibua na hakujulikana, Ami Ninje, Charles Boniface akamuibua Adi Yussuf anayechezea Grimsby Town ya England japo Chad walijitoa na kuiharibia Tanzania, hatukumuona kucheza, lakini Adi anacheza England.

Tunawaamini wachezaji wetu wa ndani, lakini miaka yote hawajaonyesha kuwa wanaweza na zaidi ni kutokana na muundo wa uendeshaji wa ligi na aina ya timu na wachezaji. Ligi ya Tanzania si imara hata kusema hatutegemei wachezaji wetu wa nje, hilo si kweli. Mikakati ifanyike, kile cha Morocco kila mmoja amekisikia, sasa isifike mahala tukaanza kujilaumu na kusema “Tumekosa wakati timu zimeongezwa.” Mechi ya Uganda inakuja Machi mwakani, tunaona ni mbali, lakini si mbali kama inavyodhaniwa. Hapo hatujaenda Cape Verde nao wako sawasawa. Lesotho wametusumbua hapa, hatujaenda kwao. Mwisho wa siku tutaanza kulaumiana, kocha hafai, wachezaji hawafai.