In Summary
  • Wanasiasa na viongozi walikuwa wanatumia utabiri wa hali ya hewa ambao sasa unatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuwaelimisha wananchi kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na aina ya mazao yanayotakiwa kupandwa kulingana na hali hiyo.

Katika miaka ya sabini na themanini tulizoea kusikia matangazo ya kuhamasisha kilimo redioni na kwenye mikutano ya hadhara. Moja ya matangazo hayo lilikuwa linasema “mvua za kwanza ni za kupandia”. Baadaye kaulimbiu hiyo ikawa sehemu ya maisha ya wakulima.

Wanasiasa na viongozi walikuwa wanatumia utabiri wa hali ya hewa ambao sasa unatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuwaelimisha wananchi kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na aina ya mazao yanayotakiwa kupandwa kulingana na hali hiyo.

TMA haitabiri kwa ajili ya wakulima tu, bali wadau wengine wanaotumia taarifa za hali ya hewa.

Mfano, utabiri wa hali ya hewa mwishoni mwa wiki umeonyesha kwamba mvua zitaendelea kunyesha pwani ya Kaskazini na TMA imetoa angalizo la uwezekano wa kuwepo na vipindi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Hata kabla ya kuanza kunyesha mvua za msimu huu, TMA ilishatoa utabiri kwa msimu huu wa vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba ukionyesha kwamba zitakuwa juu ya wastani katika maeneo kadhaa ya nchi na hiyo inatosha kwa Serikali, taasisi, mashirika ya umma na binafsi na wananchi kwa ujumla kushtuka na kuchukua hatua.

Taarifa hiyo ya TMA imebainisha athari kadhaa kwa sekta zinazohusiana zaidi na hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na chakula, mifugo na wanyamapori, maliasili na utalii, nishati na maji, mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa.

Imebainisha kuwa kwa mwelekeo wa mvua za vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.

Pamoja na matarajio hayo ya mvua za wastani katika maeneo mengi, TMA imesema kuna uwezekano wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa hususan Desemba. Pia, imetabiri mtawanyiko hafifu wa mvua na vipindi virefu vya ukavu katika baadhi ya maeneo hayo katika msimu wa mvua wa Oktoba hadi Desemba.

TMA imeshauri kuwa wakulima katika maeneo hayo waandae mashamba yao mapema na kupanda mazao yanayokomaa katika muda mfupi. Imezikumbusha mamlaka husika, kama vile wadau wa afya, menejimenti za maafa, mamlaka za miji na wadau wengine, kuchukua hatua stahiki katika kupunguza athari mbaya zinazoweza kutokea katika msimu huu wa mvua za vuli za mwaka huu.

Pamoja na tahadhari ya TMA, mvua zilizonyesha hivi karibuni ni kama zimetushtukiza kwani maandalizi kwa ajili ya kukabiliana na majanga au kuzitumia kikamilifu, si kwa kiwango kinachotakiwa na ndiyo maana maeneo ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na usumbufu kwa wananchi miaka iliyopita, yameendelea kubaki vilevile.

TMA ilishauri wakulima na wafugaji kuvuna maji kwa ajili ya matumizi endelevu.

Nasi tunazikumbusha wizara husika, mamlaka za serikali za mitaa ma mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya maandalizi ya kutosha na kuhimiza wananchi kutumia mvua vizuri kwa kilimo na kuvuna maji, lakini pia kuchukua tahadhari za kujiepusha na athari za mvua.