In Summary

Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema ajali za barabarani zinapoteza maisha ya watu milioni 1.25 kila mwaka. Kwa kiasi kikubwa, ajali hizo zinazuilika.

Matukio zaidi kuongezeka sambamba na vifo pamoja na ulemavu wa kudumu kwa majeruhi. Takwimu za ndani na kimataifa zinathibitisha hilo.

Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema ajali za barabarani zinapoteza maisha ya watu milioni 1.25 kila mwaka. Kwa kiasi kikubwa, ajali hizo zinazuilika.

Kwenye maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani yaliyofanyika mkoani Geita mwaka jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni alisema kwa miaka mitatu iliyopita, kuanzia 2013 mpaka 2015 abiria 3,444 walipoteza maisha na 20,181 kujeruhiwa.

Watembea kwa miguu 3,328 walipoteza maisha kutokana na ajali hizo huku 8,256 wakijeruhiwa ndani ya muda huo wakati WHO ikisema asilimia 26 ya vifo vilivyotokea vilihusisha watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, idadi ambayo kwa Afrika ni asilimia 33.

Siyo abiria na watembea kwa miguu pekee wanaokumbwa dhahama hii. Masauni alisema wapanda pikipiki 2,493 walipoteza maisha na 10,702 walijeruhiwa. Watumia baiskeli 1,071 walipoteza maisha 2,060 kujeruhiwa. Walikuwapo pia wasukuma mikokoteni 81 waliofariki na 246 waliojeruhiwa.

Ni taarifa zisizopendeza kwa kuzingatia jinsi zinavyoumiza nyoyo za wengi wanaoondokewa na ndugu, jamaa na marafiki wao.

Pamoja na haya yote siridhishwi na taarifa zinazotolewa na Jeshi la Polisi kupitia kitengo chake cha usalama barabarani. Mara nyingi, sababu hujirudia hivyo huniongezea shaka.

Mwendokasi. Kama wanaambizana hivi hawa makamanda wa mikoa na wilaya. Kila ajali kubwa inayovuta waandishi wa habari, akitoa kamanda unajua tu majibu yake: ‘dereva alikuwa anaenda mwendokasi na gari likamshinda.’

Wanaweza wakabadili mpangilio wa maneno, lakini mwendo kasi lazima iwepo kuwa ni sababu ya ajali iliyopoteza maisha ya wahusika.

Jeshi litumie ujuzi wa askari wake kufanya uchunguzi wa ajali hizi. Inawezekana kutobainisha vyanzo halisi ndiko kunakochelewesha upatikanaji wa ufumbuzi.

Mwendokasi wa askari hawa huwa hauna kipimo. Hawasemi gari husika lilikuwa linaendeshwa kwa kilometa ngapi kwa saa na uwezo wake ni upi na barabara husika inataka dereva aendeshe kwa mwendo upi. Wanaacha maswali mengi kwa wanaowasikiliza.

Wapita njia ndiyo wanaotegemewa kutoa taarifa za awali ambazo pia huhitimisha uchunguzi wa askari hawa. Ningependa utaratibu ubadilike. Wakati mpita njia anapoona gari linaenda kasi kama itakuwa ndiyo sababu hasa askari aje atuambie hiyo kasi inahusikaje na ajali.

Kwa sababu, kwa kawaida, gari yenye uwezo wa kutembea zaidi ya kilometa 200 kwa saa ikiendeshwa kwa kilometa 120 kwa saa itakuwa kwenye mwendo kasi, lakini siyo lazima ipate ajali kwani ipo ndani ya vipimo vyake vya kawaida. Hivyo, ikipata ajali sidhani kama mwendo huo utakuwa sababu pekee.

Huwa hatuambiwi mfumo wa usukani, mafuta, umeme, gia au mingine imechangia vipi ajali yoyote isipokuwa mwendo kasi.

Mara kadhaa, kampuni kubwa za utengenezaji wa magari zimetangaza kukosea moja ya mifumo hii hata kuitisha magari yaliyouzwa kwa wateja wake ili wayafanyie marekebisho.

Licha ya ukweli huo, tunafahamu uwezo wa nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, magari mengi ni mitumba bado wamiliki hawazingatii matengenezo kama inavyoshauriwa.

Kutotimiza wajibu huu wa kupeleka gari gereji kwa wakati ili kulifanyia matengenezo muhimu, inaweza kuwa sababu ya ajali ambayo haisemwi au inatajwa mara chache.

Ripoti ya WHO ilionyesha asilimia 80 ya magari yaliyouzwa mwaka huo hayakufikia viwango vya msingi vya usalama hasa katika nchi maskini. Siyo magari pekee, tunanunua mitumba ya pikipiki na baiskeli pia ambazo kutokamilika kwake kiufundi kunaweza kusababisha ajali.

Niwaombe trafiki wawe kama daktari ambaye huwezi kwenda kwake ukasema unahisi maumivu ya kichwa au viungo, uchovu na joto kali, hivyo akupe dawa za malaria. Lazima akupime kujiridhisha kwani hizo zinaweza kuwa dalili za ugonjwa mwingine kama vile maambukizi ya njia ya mkojo.

Mwendokasi ni dalili siyo sababu ya ajali, ninavyo amini. Vinginevyo taarifa za ziada kwenye mwendo huo zitolewe. Ielezwe imekuwaje mwendo huo ukasababisha ajali.

Ndiyo, tunawaona wakimbiza magari au pikipiki, wanaendesha mwendo mkubwa, mara nyingi zaidi ya kilometa 100 kwa saa, lakini hawapati ajali kwa kuwa wanakuwa ndani ya uwezo wa vyombo vyao.

Julius ni mwandishi wa Mwananchi. Kwa maon na ushauri, anapatikana kwa 0759 354 122