In Summary

Ni kituo ambacho kimechangia katika kuwaibua vijana wengi kama akina Thomas Ulimwengu na wengine wengi hivyo kuweza kuyafikia malengo waliyokusudia. Kwa mdau yeyote anayefika katika kituo hicho pale Karume, atagundua kwamba kuna mambo ambayo hayako sawa kutokana na haya yafuatayo:

Ukifika Uwanja wa Karume siku za Jumamosi na Jumapili utakuta vijana wakiwa wamejumuika kwa wingi katika umri tofauti wakiwa na shauku ya kupata misingi mizuri ya kuucheza mpira wa miguu.

Ni kituo ambacho kimechangia katika kuwaibua vijana wengi kama akina Thomas Ulimwengu na wengine wengi hivyo kuweza kuyafikia malengo waliyokusudia. Kwa mdau yeyote anayefika katika kituo hicho pale Karume, atagundua kwamba kuna mambo ambayo hayako sawa kutokana na haya yafuatayo:

Ile idadi ya vijana ambayo inakuwepo Karume ni kubwa kiasi kwamba kundi kubwa la wachezaji hao wanakuwa wapo wapo tu bila ya kuwa na wasimamizi wala uangalizi wa karibu na hivyo kutopewa maelekezo stahiki tangu wakiwa na umri mdogo. Kutokana na idadi hiyo, vijana hawapati maelekezo ya kiufundi ya kutosha.

Idadi ya wasimamizi pia ni chache jambo ambalo siadhani kama vijana wanaopoteza muda wao wa mwisho wa juma kama wanakipata kile walichokusudia. Idadi hiyo inapokuwa ndogo unawakuta baadhi ya wachezaji ndani ya uwanja wakicheza wenyewe bila kupata maelekezo yoyote na kama watayapata, wanaachwa waendelee kucheza wenyewe!.

Nini kifanyike

Kwa kuwa eneo la uwanja ni dogo na idadi ya vijana ni kubwa wenye umri tofauti, nashauri kwamba vijana wenye kundi la umri tofauti wafanye mazoezi siku tofauti. Hilo likifanyika, makocha wanaweza kuwa na mpangilio wenye mwendelezo ili kuona maendeleo ya vijana wanaowafundisha hatua walizozifikia. Aidha katika siku hizo mbili, kutokana na umri wao, waliowengi lazima wafundishwe vitu vya msingi kwanza (yaani ‘teknik na siyo tactic’).

Mambo kama matumizi sahihi ya sehemu zote za mwili ndiyo msingi mkubwa wa kuanza nao mchezaji wa umri huo. Hayo yanaweza kufanyika kwa ufanisi kwa kutumia eneo dogo la uwanja na hilo linawezekana kwa kutengeneza viwanja vinne ndani ya uwanja uliopo sasa na hivyo vijana kuwa na muda mwingi wa kucheza na kujifunza.

Uwanja wa mchanga kutumika

Pale Karume, ule uwanja wa mchanga unaweza kutumika kwa vijana ambao tunataka kuwajengea uelewa wa mpira wa ufukweni. Kama ilivyo kwa mpira wa miguu wa kawaida, mchezo wa ufukweni pia unatakiwa uanzie katika umri huo.

Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kama mchezo huo utasisitizwa pia. Kama wakianza kuwafundisha katika umri mdogo, watakuwa wamewajengea weledi wa mchezo huo hivyo kuja kuwa na timu ya taifa bora. Makocha wa timu za Taifa za ufukweni wanapata tabu kuwa na timu nzuri kwa sababu wachezaji wao wamejifunza ukubwani.

Idadi ya makocha iongezeke

Kama nilivyosema hapo awali, idadi ya makocha waliopo pale ni kidogo ikizingatiwa pia wingi wa wachezaji na uwiano wa kocha na idadi ya wachezaji ni mkubwa mno. Kituo hiki cha Karume kwa bahati nzuri kiko kwenye eneo ambalo lina makocha wengi wazuri na wenye uzoefu wanaoishi Dar es Salaam ambao wangeweza kwenda pale Karume na kusaidia, naamini hata bila malipo.

Hili linawezekana kwa Mkurugenzi wa Ufundi kwa kushirikiana na uongozi wa TAFCA kuwaita makocha waliopo Dar na kuliweka pendekezo hilo mbele yao, najua hawatakosekana makocha ambao watakuwa tayari kujitolea. Hata hivyo, ni vyema TFF iakawa na bajeti maalumu kwa ajili ya kituo hicho.

Kituo kuwa cha mfano

TFF itambue kwamba kituo hiki na kile cha Jakaya ndivyo ambavyo vinaonyesha taswira ya mpangilio wa kuendeleza wachezaji mpira wenye vipaji na hivyo ni muhimu kuwa katika mpangilio mzuri. Matarajio yangu ni kwamba kwa mgeni yeyote anayekuja kutembelea Dar na angependa kuona maono yetu ya mpira wa miguu, ataulizia ni wapi anaweza kuona mazoezi ya timu za vijana.

Haya yafanyike, yanawezekana na naamini kituo kitaweza kutoa wachezaji wengi ambao klabu za VPL zinaweza kuwasajili.