In Summary

Ulazima wa kuandika tena suala hili leo unatokana na kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoitoa bungeni Dodoma Alhamisi iliyopita kuwa kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa wananchi.

Miongoni mwa mambo ambayo tumeandika mara nyingi tukizungumzia umuhimu wake ni suala la Katiba Mpya. Hata leo tunalazimika kuandika tena tukiamini kwamba Katiba Mpya ni muhimu na inapaswa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.

Ulazima wa kuandika tena suala hili leo unatokana na kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoitoa bungeni Dodoma Alhamisi iliyopita kuwa kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa wananchi.

Waziri Mkuu alikuwa anajibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuhusu Katiba Mpya baada ya kukwama miaka mitatu iliyopita.

Majibu wa Waziri Mkuu ni mwendelezo wa msimamo wa viongozi wakuu wa Serikali baada ya kauli ya Novemba 4, mwaka jana aliyoitoa Rais John Magufuli alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa lilikuwamo la mchakato wa kupatikana Katiba Mpya na majibu yake yalikuwa kwamba hicho si kipaumbele chake na hakuna pahali alipoahidi kuwa atauendeleza mchakato huo.

Kama mchakato wa Katiba Mpya ulivyokuwa muhimu wakati unaanzishwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, bado tunaamini ni muhimu hata sasa na pengine ndiyo sababu hata Chama cha Mapinduzi kiliiweka katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ibara ya 145 kifungu (g).

Kifungu hizo kinasema, “Ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji, katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015-2020), CCM itahakikisha “Inakamilisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.”

Kwa kuwa mambo yote ambayo Serikali inafanya ni utekelezaji wa ilani ya CCM, na hili la Katika Mpya litatekelezwa kwa sababu ni miongoni mwa mambo ambayo yaliwashawishi wananchi waichague.

Ni kutokana na umuhimu huo hata wadau wa Katiba wamejitokeza kujadili kauli hiyo ya Waziri Mkuu wakionyesha umuhimu wa kukamilisha mchakato wa wake ama kwa kuanzia pale ulipokomea kwenye Katiba Inayopendekezwa au kurudi nyuma kuanzia kwenye rasimu ya Jaji Joseph Warioba.

Wadau hao wakiwamo wanasiasa na wanaharakati wanasema suala la fedha si kigezo, bali suala la msingi ni kwamba Watanzania wanataka Katiba Mpya

Mathalani, mmoja wa wadau hao, anasema hata kama kuna huduma za jamii, hii ya Katiba ni nyeti kuliko kitu chochote na inatakiwa ipatikane inayofanana na wakati tulionao badala ya hii ya sasa ambayo tumetoka nayo kwenye mpito wa chama kimoja kwenda vyama vingi.

Vilevile, wanasema Katiba Mpya ilishapewa kipaumbele na wananchi na ndiyo maana walijitokeza kwa wingi kutoa maoni wakati mchakato ulipoanza.

Tunaamini Katiba Mpya ni jambo la msingi kwani itasaidia kuifanya kazi ya kusafisha nchi aliyoianza Rais Magufuli kuwa rahisi kwa kuweka sawa mifumo ya uendeshaji nchi kwa ajili ya kukabiliana na mazingira ya sasa na ya baadaye.

Lakini yote kwa yote, tunahofia tusije kuingia katika mtego wa mchakato wa Katiba kuishia tena njiani na hivyo kupoteza mabilioni ya fedha za walipakodi kama ilivyokuwa katika mchakato wa awali. Hivyo, tunamshauri Rais aliingize suala hili katika vipaumbele vyake kama ilivyo kwa vipaumbele vingine vya ilani ya CCM.