In Summary
  • Ni kweli. Wakati mwingine umehenya kwa miezi mitatu, sita, hata mwaka, ukitafuta taarifa na vyanzo makini. Lakini dakika chache baada ya kazi yako kuingia sokoni; kwa kutangazwa au kuchapishwa gazetini, tayari kuna ujumbe, ama wa kukosoa, kukana, kushutumu, kufafanua, kuelimisha au kupongeza.

Mara nyingi utasikia waandishi wa habari wakisema “ubaya” wa kazi hii ni hukumu ya papohapo. Kwamba uliandika jana. Taarifa au habari zikachapishwa katika toleo la leo. Saa 12 asubuhi msomaji wa gazeti anapiga simu “kukuonyesha kasoro.”

Ni kweli. Wakati mwingine umehenya kwa miezi mitatu, sita, hata mwaka, ukitafuta taarifa na vyanzo makini. Lakini dakika chache baada ya kazi yako kuingia sokoni; kwa kutangazwa au kuchapishwa gazetini, tayari kuna ujumbe, ama wa kukosoa, kukana, kushutumu, kufafanua, kuelimisha au kupongeza.

Ni haya – kukosoa, kukana, kushutumu, kufafanua, kuelimisha au kupongeza – ambayo hufanya waandishi wa habari wawe makini zaidi katika kutafuta ukweli, usahihi na uthibitisho wake.

Ndivyo ilivyokuwa katika Mwaka Mpya. Matoleo ya gazeti hili ya tarehe 2 na 3 Januari 2018 yamedakwa na wasomaji kwa kasi ya moto wa kiangazi. Wanatushangaa. Wanatusahihisha. Wanatukosoa. Wanatukemea. Wengine wanajenga shaka juu ya uwezo wetu.

Msomaji mmoja amejadili habari ya ukurasa wa mbele toleo la 3 Januari yenye kichwa ‘Sugu ahojiwa polisi kwa maneno ya uchochezi.’

Wasomaji wanne wamejadili habari ya ukurasa wa mbele, tarehe 2 Januari yenye kichwa kisemacho: ‘Miji iliyopokea Mwaka Mpya nyakati tofauti.’

Wengine kumi na mmoja (11) wamejadili habari ya ukurasa wa mbele, 3 Januari yenye kichwa kisemacho: ‘Maofisa wa TRA wamhoji Askofu Kakobe kwa saa sita.’

Tuanze na msomaji mmoja aliyejadili habari, ‘Sugu ahojiwa polisi kwa maneno ya uchochezi.’ “Hii siyo mara ya kwanza kuona mnaandika hivi; lakini nadhani mnakosea. Ukiandika ‘ahojiwa polisi kwa maneno ya uchochezi,’ ina maana hata wewe tayari unakubali ni maneno ya uchochezi wakati uchochezi unapaswa kuthibitishwa mahakamani.”

“Hapa, ama mnakuwa mashabiki au mnachukua kauli ya polisi bila uthibitisho. Bora kuandika ahojiwa kusema hili na lile – ukitaja alichosema kuliko kutoa hukumu,” ameeleza msomaji.

Mmoja wa wasomaji wanne waliojadili habari ya ‘Miji iliyopokea Mwaka Mpya nyakati tofauti’ anauliza, “Je, miji ilikuwa inashindana kuona ni upi utakuwa wa kwanza? Kwani ilikuwaje mwaka jana, mwaka juzi na miaka yote huko nyuma?”

Wengine wawili, mmoja aliuliza, “Kwani ukienda Mashariki unatokezea wapi? Kwani Mashariki inaishia tu pale wanakotaja kunaanza kupambazuka?” Mwingine anaandika, “…kuna haja ya kumfufua Galileo Galilei kutueleza mzunguko wa dunia?”

Msomaji wa nne anaandika, “Mimi siyo mwandishi wa habari; lakini hii siyo habari. Wangeandika kuwa kumekucha kwanza New Delhi au Dar es Salaam, hiyo ndiyo ingekuwa habari maana ni kinyume na mfumo wa siku zote.”

Galileo Galilei (1564–1642), alikuwa mwanafizikia na mwanafalaki (mwenye elimu ya sayari) aliyepewa kifungo cha maisha gerezani na baadaye kufungiwa nyumbani kwake kutokana na ugunduzi wake kuwa dunia huzunguka jua.

Ugunduzi huo ulikinzana na imani ya watawala chini ya Kanisa Katoliki wakati huo. Hata hivyo, Papa John Paul II, mwaka 1979, aliunda kamati maalum juu ya umajusi wa Galileo na kuja na tamko kuwa alikuwa sahihi; miaka 359 tangu atiwe hatiani.

Nao wasomaji 11 waliojadili habari yenye kichwa kisemacho: ‘Maofisa wa TRA wamhoji Askofu Kakobe kwa saa sita’ walikuwa katika maeneo mawili. Eneo la kwanza la wasomaji sita linadai kuwa mwandishi hakuwa sahihi kwa kuandika kuwa magari ya TRA “yaliingia kanisani.”

Mmoja wao anaandika, “Kanisa limejengwa kwa ajili ya watu, waumini. Hakuna nafasi ya kuweka magari.” Wengine watatu wanalaumu mwandishi kwa kutokuwa “makini;” mmoja wao akiandika, “…ina maana mwandishi hajui eneo la maegesho? Magari huingia kanisani kweli?”

Katika eneo la pili, wasomaji wawili wanasema mwandishi “si makini.” Mmoja anaandika “…kichwa cha habari kinataja maofisa wa TRA kumhoji askofu wetu; lakini katika habari hii kuna sehemu inaonyesha kuwa mwandishi alimuuliza ofisa elimu ya umma wa mamlaka hiyo kama waliokwenda kanisani ni wa TRA, akajibiwa kuwa hana uhakika. Sasa hiyo si ndiyo ingekuwa habari?”

“Kama wanaopaswa kujua wanasema hawajui au hawana uhakika; na mwandishi anashindwa kuthibitisha kutoka TRA, sisi wasomaji tuelewe lipi?” anahoji mwingine.

Msomaji mwingine anahoji, “…mwandishi ameandika kuwa ofisa ‘ameshindwa kukubali au kukataa…’ Mimi msomaji nielewe nini hapa. Si angetuandikia alichokubali au alichokataa? Hamuwafundishi kuhoji?”

Meza ya Mhariri wa Jamii itaendelea kutoa fursa kwa wasomaji kutoa maoni juu ya uandishi na waandishi katika vyombo vya MCL. Wewe una maoni gani juu ya yaliyowasilishwa?