In Summary

Ni kipindi kizuri cha mavuno kwa mchezaji ambaye amefanya kazi nzuri uwanjani na mchango wake umeonekana hadharani siyo vinginevyo.

Msimu wa usajili majira ya kiangazi unakaribia kwa wanasoka wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya kuvuna fedha za maana kulingana na thamani zao.

Ni kipindi kizuri cha mavuno kwa mchezaji ambaye amefanya kazi nzuri uwanjani na mchango wake umeonekana hadharani siyo vinginevyo.

Thamani ya mchezaji itaonekana uwanjani kwa mchango aliyotoa katika mechi za ushindani ambazo zimechangia timu yake kupata matokeo mazuri.

Kila kocha ana kiu ya kupata mafanikio katika kazi yake, lakini msingi mzuri wa kujenga jina unatokana na kiwango bora cha wachezaji wake.

Kocha anaweza kusajili kwa nia njema akiwa na matumaini ya kupata mafanikio, lakini matarajio yake yanaweza kuwa tofauti na hata kufikia hatua ya kuigharimu.

Wakati klabu za Ulaya zikipigana vikumbo kuhusu usajili wa majira ya kiangazi, dirisha dogo hapa kwetu linatarajiwa kufunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15.

Ni kipindi mwafaka kwa makocha kufanya usajili mdogo wa kuziba viraka wakati ligi ikiwa katika mzunguko wa kwanza kwa kuongeza au kubaki na wachezaji wake wa awali kulingana na mahitaji.

Tofauti na makocha wa Ulaya, usajili wa hapa bongo umegawanyika katika makundi mawili bila kujali uhalisia wa mahitaji ya benchi la ufundi.

Klabu zetu zimeweka ‘utaratibu’ wa kusajili wachezaji kutokana na presha ya mashabiki ambao wakimtaka mchezaji wao kocha hana sauti.

Ni utamaduni kwa klabu za Simba na Yanga kusajili mchezaji kwa shinikizo la mashabiki vinginevyo kocha au kiongozi aliyepo madarakani atafungashiwa virago mchana kweupee!

Dhana hii inaendana na mfumo wa klabu hizi kusajili kwa kukomoana. Tuliona mfano katika usajili uliopita kwa kiungo Pius Buswita.

Tunajua kilichotokea katika usajili wa Buswita aliyetua Yanga kutoka Mbao FC kabla ya miamba hiyo kukaa meza moja kumalizana nje ya utaratibu.

Presha ya mashabiki mara nyingi inamtoa kocha kwenye utaratibu wake wa kujenga timu imara ya ushindani kulingana na mahitaji ya kujaza husika.

Wakati mwingine kocha analazimika kutekeleza matakwa ya mashabiki kusajili mchezaji asiyekuwa na mpango naye kwasababu ya kuhofia kitumbua chake kuingia mchanga.

Presha ya mashabiki mara nyingi imekuwa ikiziondoa mchezoni Simba na Yanga na hapo ndipo linapoibuka zengwe la kudaiwa kocha hana uwezo na mwisho wa siku anatupiwa virago.

Baadhi ya makocha wamepoteza kazi kutokana na shinikizo la mashabiki ambao wamekuwa na sauti kubwa.

Kwa bahati mbaya sana viongozi wengi wanaongoza klabu za soka wanashindwa kufuata msingi wa utawala bora kutokana na sababu zao binafsi.

Kwa kutokujiamini kwao kumechangia viongozi wengi kuingilia majukumu ya benchi la ufundi na wengine wamefikia hatua ya kumpangia kocha kikosi.

‘Utaratibu’ wa viongozi wa klabu kukiuka misingi ya uongozi unatoa nafasi kwao kuingilia hata masuala ya kiutendaji kwa kocha ikiwemo usajili wa wachezaji.

Kocha hana sauti mbele ya kigogo akitaka ‘mchezaji’ wake asajiliwe bila kujali mahitaji ya timu kwa wakati husika au kiwango chake uwanjani.

Pia ni kipindi cha ulaji kwa baadhi ya viongozi wa klabu ambao wamekuwa na ‘utaratibu’ wa kuingia makubaliano na mchezaji husika kwa lengo la kupata ‘ten parcent’.

Ni katika utaratibu huo utamkuta kiongozi anatokwa povu kuhakikisha mchezaji anayemtaka anasajiliwa kwa gharama yoyote ili kuhakikisha anatimiza malengo ya kupata ‘mzigo’.

Tumewahi kusikia kiongozi akimtaka kocha kumpanga mchezaji fulani kwa sababu tu yeye ndiye anayemlipa mshahara na posho za kuishi mjini.

Mfumo waliozoea viongozi wa klabu hizo umeshindwa kutoa matunda mazuri na mwisho wa siku zigo la lawama anatwishwa kocha endapo timu itaboronga katika mechi zake.

Wakati umefika kwa mfumo wa uendeshaji wa klabu ubadilike kuanzia kwa viongozi ili kuzipa timu mafanikio katika michuano mbalimbali.

Ni wakati mwafaka kwa viongozi kumpa uhuru kocha kujenga timu yake kwa kuchagua aina ya mchezaji anayemtaka kulingana na mahitaji.

Kocha ni mtu wa kwanza kuwajibika timu inaposhindwa kupata mafanikio, hivyo ni vyema akapewa nafasi ya kujenga timu ili atakapoharibu iwe rahisi kumuhukumu kwa matokeo inayopata timu katika mechi zao.

Endapo hakutakuwa na mabadiliko ya kiutendaji kwa makocha kupewa uhuru wa kuchagua wachezaji wanaotaka, itakuwa ndoto Tanzania kupiga hatua katika medani ya soka.

Dirisha dogo la usajili linawadia, makocha wapewa fursa ya kuchagua wachezaji wanaotaka ili kujenga timu imara ya ushindi.

Kocha akipewa uhuru huo hatakuwa na kisingizio timu itakapofanya vibaya katika michuano.