In Summary
  • Hata hivyo, inasikitisha kuwa Watanzania wengi walioajiriwa katika sekta hiyo, wanalima kwa ajili ya kujikimu tu.
  • Miongoni mwa sababu zinazokwamisha ukuaji wa wakulima wa Tanzania ni kutojengewa mazingira ya kibiashara ya mazao wanayolima.

Kilimo ni njia kuu ya uchumi wa Tanzania, ikiajiri zaidi ya asilimia 70 ya wananchi.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa Watanzania wengi walioajiriwa katika sekta hiyo, wanalima kwa ajili ya kujikimu tu.

Miongoni mwa sababu zinazokwamisha ukuaji wa wakulima wa Tanzania ni kutojengewa mazingira ya kibiashara ya mazao wanayolima.

Tumezoeshwa tangu enzi za ukoloni kwamba mazao ya biashara ni yale yasiyo ya chakula kama katani, kahawa, chai, pareto na korosho.

Kumbe hata mazao ya chakula kama nafaka jamii ya mikunde, mbegu za mafuta na matunda ni biashara inayoweza kuwakwamua wakulima kutoka kwenye lindi la umasikini.

Wakulima wengi wamehamasika kulima mazao ya chakula na kuuza ziada baada ya kutoa akiba inayowatosha, lakini changamoto imekuwa ni masoko.

Serikali, ambayo ni kama mlezi wa wakulima, imegeuka kuwa kikwazo cha masoko kwa kuwakataza wakulima wasiuze mazao yao nje ya nchi kuepuka njaa.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba aliyoitoa wakati wa Bunge la Bajeti, tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kwa msimu wa 2015/2016 na upatikanaji wa chakula 2016/2017 iliyofanyika mwezi Julai 2016, ilibainisha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia tani milioni 16.2 na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2016/17 ni tani milioni 13.2, hivyo nchi kuwa na ziada ya tani milioni 3.01.

Kati ya ziada hiyo, tani milioni 1.1 ni za mazao ya nafaka na tani milioni 1.9 ni za mazao yasiyo nafaka. Nchi ilikuwa na kiwango cha utoshelevu wa kiwango cha asilimia 123 ikilinganishwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 120 kwa mwaka 2015/2016.

Pamoja na ziada yote hiyo ya chakula, bado wakulima na wafanyabiashara hawaruhusiwi kuuza mazao nje ya nchi. Kwa hali hiyo wakulima watajikwamuaje kutoka kwenye umasikini? Wakati uzalishaji wa chakula ukipitiliza, uwezo wa Serikali kuhifadhi chakula ni mdogo. Takwimu hizo za waziri zinaonyesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/2017 umepanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula. Hiyo ni sawa na asilimia 0.62 ya chakula kinachozalishwa kwa mwaka.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa uwezo wa Serikali kuhifadhi chakula ni mdogo. Matokeo yake, kazi ya kuhifadhi chakula sasa imewekwa kwa mkulima mdogo ambaye anapangiwa masoko ya kuuza chakula bila kujali gharama alizotumia kuzalisha. Hali hii inaweza kuwakatisha tamaa wakulima wadogo na hata wale wakubwa wanaowekeza kwenye kilimo.

Watanzania wengi wamejikita kwenye kilimo, lakini linapofika suala la masoko mtu anajiuliza mara mbili.

Kwa kuwa Serikali ndiyo yenye jukumu la kulinda usalama wa chakula, ipeleke chakula kwenye maeneo yenye upungufu, ili wakulima wanaovuna chakula cha kutosha wawe huru kuuza wanakotaka.

Mbali na masoko, Serikali pia iwajengee uwezo wakulima wa jinsi ya kuhifadhi mazao yao kwa kuwa wanatumia nguvu nyingi kulima, kupanda, kutunza mazao, lakini mwishowe yanaishia kuoza.

Wadau wa kilimo washirikishwe katika kutoa mbinu bora za kuhifadhi chakula wakati suala la masoko nalo likiwekewa mkakati madhubuti. Kama Serikali itawahakikishia wakulima masoko ya uhakika ya mazao yao, watu wengi watashawishika kujiajiri kwenye kilimo na hapo ndipo tutakapoona mfumuko wa viwanda vya kusindika mazao. nchini, lakini huo usiwe mzigo wa kuwakwaza.

0754 897 287