In Summary
  • Kwa wengi, aghalabu uzoefu wangu unaonyesha maswali yao mengi huelekezwa kwa Serikali.
  • Hawa wanaamini kwa kuwa hao wasiojua kusoma na kuandika wengi wanatoka katika shule za umma, Serikali haina namna ya kukwepa lawama hizi.

Zinapotoka taarifa kuwa maelfu ya wahitimu wa darasa la saba hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu, unajiuliza maswali kadhaa.

Kwa wengi, aghalabu uzoefu wangu unaonyesha maswali yao mengi huelekezwa kwa Serikali.

Hawa wanaamini kwa kuwa hao wasiojua kusoma na kuandika wengi wanatoka katika shule za umma, Serikali haina namna ya kukwepa lawama hizi.

Ukubwa ni jalala na kwa vile Serikali ndiyo mdau mkubwa wa elimu, lazima ikubali hali hiyo na kuichukulia kama changamoto.

Inatia moyo kuwa katika miaka ya karibuni, Serikali imeamua kwa dhati kuifanyia kazi changamoto hii.

Utekelezaji wa mipango kama ule wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (Lanes), ni ushahidi tosha wa namna Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilivyoamua kulivalia njuga tatizo la wanafunzi wa elimu ya msingi kutojua stadi hizo muhimu maishani.

Kwa kawaida mtoto anayefika darasa la tatu anapaswa awe ameshajua stadi hizi.

Hata hivyo, hali haiko hivyo. Tafiti mbalimbali, zikiwamo zinazotolewa na asasi ya Twaweza kila mwaka zinaonyesha baadhi ya wanafunzi wanavuka darasa hilo pasipo kuwa na stadi hizi.

Kwa mfano, tathmini ya Uwezo iliyo chini ya Twaweza ya mwaka 2015 ambayo ripoti yake ilizinduliwa mwaka huu, kati ya watoto 10, wanne walibainika kutokuwa na uwezo wa kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Nimesema hapo mwanzoni kuwa Serikali imeshakiri kuwapo kwa udhaifu huu na ndiyo maana sasa inajihimu kutekeleza mipango mbalimbali ukiwamo huu wa kukuza stadi za wanafunzi kusoma kuandika na kuhesabu, maarufu kwa kifupicho cha KKK.

Kwa hakika matunda yameshaanza kuonekana na kama tutajipanga vizuri kwa wadau wote, wakiwamo wazazi, uko uwezekano mkubwa wa tatizo hili kuwa historia.

Hivi karibuni, nilikuwa katika ziara ya wanahabari waliokwenda katika baadhi ya mikoa kujionea hali halisi shuleni.

Ni ziara iliyolenga kuangalia utekelezaji wa baadhi ya miradi ya elimu nchini ikiwamo huu wa KKK na ule wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R).

Kimsingi, hali inatia moyo; pamoja na changamoto za kiutendaji, walimu katika shule tulizotembelea wanakiri mafunzo waliyopata yanawasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika.

Mathalan, mwalimu mwenye wanafunzi wapatao 160 darasani, hivi sasa anasema ifikapo mwisho wa mwaka, wanafunzi wanaoshindwa kusoma wanaweza kuwa chini ya 40 na hao ni wale watoro au wenye matatizo ya uelewa.

Haya si mafanikio ya kubeza; juhudi hizi zinapaswa kuimarishwa na kulindwa kwa mustakabali wa elimu yetu.

Hata hivyo, kinachosikitisha ni kuona kuwa baadhi ya watu, wanataka kuturudisha nyuma.

Kwa mfano, ukiondoa wingi wa wanafunzi darasani, changamoto kubwa iliyopo ni wanafunzi kukosa chakula.

Ukweli ni kuwa penye njaa shule ‘haipandi’.

Ilitegemewa suala la njaa lifanywe kuwa kipaumbele kuanzia kwa wazazi, viongozi na jamii kwa jumla.

Lakini hali haiko hivyo. Tulipotembelea Shule ya Msingi Endaberg iliyopo mkoani Manyara, walimu walilalimika kuwa itikadi za kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, zinakwamisha mchakato wa utoaji chakula kwa watoto.

Shule hii ni mfano mmoja; ukweli ni kuwa katika maeneo mengi harakati nyingi za ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo, zinakwazwa na wanasiasa wanaohamasisha watu wasishiriki.

Kwa mfano, mara kadhaa kumeripotiwa taarifa za wanasiasa wa upinzani wakiwakataza wananchi kushiriki katika miradi ya elimu kwa hoja kuwa hilo ni jukumu la Serikali.

Vivyo hivyo, katika maeneo yaliyo chini ya upinzani, wanasiasa wa CCM wanafanya kampeni ya kudhoofisha harakati za maendeleo zinazobuniwa na upinzani.

Kwa shule kama Endaberg na nyinginezo, wasichokijua viongozi wa CCM na Chadema ni kuwa mvutano wao unawaaathiri watoto wao.

Wanaweza kufikiri wanakomoana, lakini ukweli ni kuwa wanaoumia ni watoto wao. Na hapa ndipo unapopima uwezo wa kufikiri wa baadhi ya viongozi wetu wa siasa. Kwangu huu ni uduni wa fikra uliovuka mipaka.

Tanzania ni zaidi ya itikadi ya vyama na kama kuna maeneo ambayo tunahitaji kuepuka siasa hasa hizi zisizo na tija, ni pamoja na sekta ya elimu.

Tuvurugane, tupingane kwingine, lakini katu tusiingize tofauti za kivyama katika elimu ambayo ni sekta mama kwa maendeleo ya Taifa.

Abeid Poyo ni mwandishi wa Mwananchi. Anapatikana: makala@mwananchi.co.tz