In Summary
  • Chini ya mfumo wa zamani, klabu ilikuwa inamilikiwa na wanachama kwa asilimia 100. Wanachama hao ndio waliokuwa na mamlaka yote ya uendeshaji klabu na hivyo walikuwa wakikutana kila baada ya miaka minne na kuchagua viongozi wao.

Jana, mkutano mkuu wa klabu ya Simba ulipokea taarifa za mshindi wa zabuni ya kununua asilimia 50 ya hisa za klabu na hivyo kubariki mabadiliko ya mfumo wa umiliki klabu, ambao pia utabadili mfumo wa uendeshaji.

Chini ya mfumo wa zamani, klabu ilikuwa inamilikiwa na wanachama kwa asilimia 100. Wanachama hao ndio waliokuwa na mamlaka yote ya uendeshaji klabu na hivyo walikuwa wakikutana kila baada ya miaka minne na kuchagua viongozi wao.

Katika mfumo huo, wanachama walikuwa wakimchagua rais, makamu wake na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambayo pia ilikuwa inatakiwa kuwasilisha majina ya wtu wanaopendekezwa kuwa wadhamini wa klabu.

Mfumo huo ulianza vizuri kutokana na wanachama wa awali kuzingatia maslahi ya klabu na hivyo kutafuta watu waliokuwa na uwezo na kuwashawishi kugombea uongozi.

Wale waliokubali pia walihakikishiwa msaada kutoka kwa wanachama na hivyo klabu hizo kujiendesha vizuri kwa takriban robo tatu karne. Hata hivyo katika miaka ya karibuni, wajanja waligundua kuwa klabu hizo zina fursa nyingi.

Baadhi waliamua kuingia katika uongozi kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, wengine kujilinda, wengine kuwa na malengo ya kisiasa na wengine kujinufaisha kifedha.

Hii ilidumaza maendeleo ya klabu na ukweli kwamba wanachama ndio waliokuwa na sauti ya mwisho, ulisababisha wajanja watumie mianya ya katiba kuyumbisha viongozi kwa maslahi binafsi.

Matokeo yake migogoro ilikuwa haiishi. Kila wakati timu isipofanya vizuri, matatizo yakawa na viongozi na suluhisho kuwa ni waondolewe..

Migogoro hiyo ilisababisha klabu kuanza kufikiria kubadilisha mfumo wa umiliki na uendeshaji. Lakini hata juhudi hizo zilikwamishwa na wanachama wachache waliokuwa na maslahi binafsi.

Lakini baada ya vikwazo vyote hivyo, Simba imefanikiwa kubadilisha mfumo wake na jana mmoja wa wanachama wake maarufu, Mohamed Dewji alipitishwa kuwa mshindi wa zabuni ya mwanahisa mbia katika umiliki wa klabu.

Haya ni mafanikio makubwa ambayo kama yatetekelezwa vizuri yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika michezo.

Kwa hiyo, uongozi na wanachama wa Simba wanastahili pongezi kubwa kwa kufanikisha mabadiliko hayo ili klabu ianze kuendeshwa kisasa badala ya mfumo uliopo sasa unaotumiwa vibaya.

Tunajua kuwa safari hiyo ya mabadiliko haijaishia katika kumjua mshindi tu, bali inaendelea hadi hapo wanachama watakapoelewa vizuri mfumo mpya unafanyaje kazi.

Tunaelewa kuwa katika kipindi cha mpito, kutakuwepo na mabadiliko mengi ambayo hayajazoeleka kwa wanachama na viongozi. Wapo viongozi ambao watapoteza nafasi zao, wapo waajiriwa ambao watakosa sifa za kuwa katika ajira ya klabu inayoendeshwa kisasa na wapo wanachama watakapoteza nguvu na ushawishi wao kutokana na mfumo mpya.

Cha msingi ni wote kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, kuangalia kwa makini uzuri na kasoro za mfumo huo na kutopoteza mwelekeo wa dhamira iliyosukuma mabadiliko hayo. Wanachama wakiungana kusaidia mabadiliko haya, watakuwa wameleta mabadiliko katika sekta nzima ya michezo na si Simba pekee.