In Summary

Dk Shein ameyazungumza hayo leo Ijumaa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja vya Amaan, visiwani Zanzibar

Dar es Salaam. Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk Mohamed Shein amesema hadi kufikia Julai mwaka huu, sera ya elimu bure itaanza kutekelezwa ili kutekeleza sera ya Mapinduzi.

Dk Shein ameyazungumza hayo leo Ijumaa wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja vya Amaan, visiwani Zanzibar.

Dk Shein amesema wakati tayari elimu ya msingi ilianza kutolewa bure, bado wanafunzi wa sekondari walikuwa wakiendelea kulipia gharama.

“Julai mwaka huu tunairudisha sera ya elimu bure kwa shule za sekondari ili kutekeleza sera ya mapinduzi, hakuna mzee ambaye atachangia elimu,”amesema Dk Shein.

Hata hivyo, amesema katika kipindi cha mwaka 2015/2017 kumekuwa na uimarikaji wa huduma za elimu ikiwemo ujenzi wa shule tisa za serikali zenye ghorofa kwa kipindi cha mwaka 2017.

Amesema japokuwa kumekuwa na changamoto katika ununuzi wa madawati, tatizo hilo litamalizika mwaka huu, lakini kinachofanywa sasa ni kuhakikisha wanarudisha utaratibu wa elimu bure.

Katika hotuba yake, Dk Shein ameainisha mambo mengi ya mafanikio ikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo karibu yote imefanya vizuri.