In Summary

Mwalimu aliyasema hayo jana wakati akitangaza washindi wa shindalo la kitaifa la usafi wa mazingira ambalo lilihusisha vipengele kadhaa kikiwemo cha matumizi ya vyoo bora.


Dar es Salaam. Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Ummy Mwalimu ameonyesha kukerwa na uchafu wa vyoo katika ofisi na taasisi za Serikali na kutaka suala hilo liangaliwe kwa umakini ili kuepusha mlipuko wa maradhi yatokanayo na uchafu.

Mwalimu aliyasema hayo jana wakati akitangaza washindi wa shindalo la kitaifa la usafi wa mazingira ambalo lilihusisha vipengele kadhaa kikiwemo cha matumizi ya vyoo bora.

Alisema licha ya kuwa watendaji wa Serikali ndiyo wanapaswa kuwa wahamasishaji wa usafi kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitumia vyoo vichafu.

Kutokana na hali hiyo Mwalimu alisema ipo haja ya kuanza kushindanisha taasisi na ofisi za Serikali katika usafi wa mazingira hasa wa vyoo.

Pia, Mwalimu aliagiza shule za msingi na sekondari nazo zishindanishwe kupata choo bora na safi.

“Kuna ofisi za umma ukienda chooni unaweza kutamani ukajisaidie barabarani kutokana na uchafu, tatizo kubwa ninaloliona Watanzania hatuzingatii mazingira na usafi wa vyoo,” alisema.

Katika shindano hilo kwa mara nyingine tena Halmashauri ya Mji wa Njombe iliibuka kidedea kati ya halmashari 73 za wilaya, miji, manispaa na majiji.

Ushindi huo ulipatikana baada ya kufanikiwa katika udhibiti wa taka ngumu, usimamizi wa sheria, udhibiti wa majitaka, uwepo wa majisafi na salama pamoja na ushirikishwaji wa sekta binafi katika usafi wa mazingira.

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha utekelezaji wa kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira katika ujenzi na matumizi ya vyoo bora.

Njombe pia iliibuka mshindi katika kipengele cha kijiji bora chenye kaya ambazo zimefanikiwa kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na sehemu za kunawia mikono kwa maji na sabuni nafasi iliyoshikwa na Kijiji cha Kanikele.