In Summary

Mazoezi ya siku 17 yanashirikisha pia maofisa watendaji wa wizara.

Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga la Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la 'ushikianao imara' yatasaidia wanajeshi wa Afika Mashariki kukabiliana na matukio yakiwemo ya ugaidi na uharamia.

Mazoezi hayo yaliyoanza Desemba 4,2017 yanahusisha watu 300 wakiwamo makamanda wa jeshi kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni wenyeji Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi.

Mazoezi hayo ya siku 17 yanafanyika katika  Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani kilichopo Kunduchi wilayani Kinondoni, Dar es Salaam. Pia, yameshirikisha maofisa watendaji wa wizara nchini.

Akifungua mazoezi hayo leo Alhamisi  Desemba 7,2017, Dk Mwinyi amesema vyombo vya ulinzi vitakuwa na uwezo kutokana na uzoefu na ujuzi waliopata.

Dk Mwinyi amesema mazoezi hufanyika kila mwaka na safari hii Tanzania imeyaandaa lengo likiwa kubadilisha uzoefu na ujuzi kwa wanajeshi wa EAC.

Mwenyekiti wa Baraza la Ulinzi na Usalama wa EAC, Adolf Mwesiga amesema wameamua kuwa na mazoezi hayo kwa sababu changamoto za hali ya usalama zinafanana katika nchi wanachama.

“Mazoezi haya yanasaidia kuwapa ujuzi wanajeshi namna ya gani wanaweza kupanga na kukabiliana na uharamia, ugaidi na majanga," amesema Mwesiga ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Uganda.

Desemba 5,2017 Mkuu wa Operesheni na  Mafunzo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania  (JWTZ ), Brigedia Jenerali Alfred Kapinga  alisema mazoezi hayo hatayahusisha milio ya risasi bali makamanda wajifungia ndani wakisubiri maelekezo kwa ajili ya utekelezaji.