Dar es Salaam. Baraza la Wazee wa Chadema limemuomba Rais John Magufuli kukutana na wazee ili kujadili mustakabali wa Taifa, hasa hali ya usalama nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, wazee hao wametaka mkutano huo uwahusishe pia viongozi wa dini, viongozi wastaafu na wazee wa vyama vingine vya siasa watakaokuwa na ujasiri wa kumshauri Rais.

Katibu Mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka alisema umefika wakati kwa Rais kuwa tayari kusikiliza, kukosolewa na kupokea ushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Alisema mkutano huo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho usalama wa nchi unaonekana kutishiwa kutokana na matukio ya watu kutekwa na kuuawa kuendelea kushamiri.

“Nchi inazidi kuvimba na watu wanahitaji kupumua ni muhimu wenye dhamana walione hili tuchukue hatua mapema kabla hatujachelewa,” alisema.

“Pamoja na hali hii ya kutishia mustakabali wa Taifa, hatuoni jitihada za wenye dhamana kufumbua macho kutafuta suluhu ya pamoja kama Taifa. Ndiyo sababu tunamuomba Rais aitikie wito huu wa wazee akutane nasi tuzungumze na kumshauri kwa lengo la kuokoa nchi yetu. Hii ni nchi yetu wote.”

Alisema mitaani wananchi wanazungumza mengi na kusema ni vyema wakasilikizwa na si kupewa vitisho.

“Haki za msingi kabisa za kikatiba na kisiasa, ikiwamo watu kukusanyika na kutoa maoni yao bado zinakandamizwa, ukandamizaji huo unashereheshwa na kauli na vitendo vya viongozi wa Serikali ambao kimsingi wanatakiwa kulinda amani,” alisema.

Waripoti polisi

Katika hatua nyingine, viongozi wawili kati ya saba wa Chadema jana waliripoti Kituo Kikuu cha Polisi, huku wakili wao, Alex Massaba akisema wengine wamekwenda Dodoma kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge.

Walioripoti ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji na naibu wake (Zanzibar), Salum Mwalimu.

“Kama unavyojua kati ya viongozi walioitwa watano ni wabunge na kwa sasa vikao vya kamati vimeanza hivyo wanapaswa kuwepo na kushiriki shughuli za kibunge,” alisema Massaba.

“Kati ya hao Dk Mashinji na Mwalimu sio wabunge ndio maana wamefika kuitikia wito na tunasubiri kupewa maekekezo. Hakuna aliyehojiwa. Wamefika hapa saa tatu asubuhi na kukaa hadi saa tano asubuhi na kuambiwa waende na kurejea Ijumaa.”

Massaba alisema baada ya kuwaeleza polisi sababu za kutofika kwa viongozi wengine, walitakiwa kuondoka na kuripoti tena Ijumaa.

Viongozi walioshindwa kufika ni mwenyekiti, Freeman Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai; naibu katibu mkuu (Bara) na mbunge wa Kibamba, John Mnyika; mbunge wa Kawe na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; Esther Matiko (Tarime Mjini) na John Heche wa Tarime Vijijini.

Februari 20, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa kwa viongozi hao siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Mwanafunzi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai hati viapo kwa mawakala wao.

Imeandikwa na Elizabeth Edward na Fortune Francis.