Mwezi uliopita nilifanikiwa kumhudumia mgonjwa mmoja wa saratani ya mlango wa uzazi katika hospitali ninayofanyia kazi.

Kwa mara ya kwanza nilipopitia taarifa za mgonjwa huyo ambaye kiumri alikua na miaka 32, nilipigwa na butwaa baada ya kugundua hajawahi kumuona daktari kwa ajili ya kupata ushauri wa kiafya tangu utoto wake hadi pale tabibu wake alipompa rufaa ya kuja kwangu baada ya kupata matatizo ya kutokwa na hedhi inayodumu kwa mrefu na kutokwa na uchafu ukeni kulikodumu kwa muda mrefu bila kukoma.

Niliingia kwenye chumba cha vipimo ambacho mwanamke huyu alikuwa ananisubiri kwa ajili ya vipimo akiwa tayari amevalia gauni la hospitali. Baada ya mazungumzo ya muda mfupi ili kumwandaa kisaikolojia kwa ajili ya vipimo, nikaanza kumfanyia vipimo vya kuchukua sampuli kutoka kwenye tishu za mlango wake wa uzazi huku nikimuuliza maswali machache “ni kwa muda gani umekuwa ukipatwa na hali hii? Unahisi maumivu yoyote ninavyoendelea na vipimo?” Wakati naendelea na vipimo, niliona kiasi fulani cha damu kikimtoka ukeni, kwa kawaida hii ni dalili ya awali kabisa ya saratani ya mlango wa uzazi; kutokana na kile nilichokuwa nakijua kutoka kwa msichana huyu, wala sikushangaa japo pia hii nisingeweza kujiridhisha kama kweli ni saratani hadi pale majibu ya vipimo vya sampuli zake yatakapokuwa tayari. Mara nyingi wanawake hawatarajii kupatwa na saratani kutokana na kukosa ufahamu wa kuepukana na vihatarishi vyake na dalili zake kuu. Mara nyingi nimekuwa nikiona wanawake huwa wanapokea kwa mshangao taarifa zinazoonyesha wana saratani hasa ya mlango wa kizazi baada ya vipimo.

Hii ni kutokana na kuzipuuzia dalili za awali kwa kudhania huenda zimesababishwa na maambukizi mengine ya kawaida yanayojitokeza kwenye mfumo wa uzazi na si saratani na hivyo kupuuzia kuwaona wataalamu wa afya kwa ajili kupatiwa ushauri na vipimo kwa wakati.

Wiki iliyofuata, msichana huyo aliporudi hospitali nilifanikiwa kumpatia taarifa ambazo japo siyo njema lakini hazikuwa mbaya sana kwamba majibu ya vipimo vyake vilidhihirisha alikuwa na saratani ya mlango wa uzazi na ilikua imeanza kwenye mlango wa kizazi bado haijasambaa. Hii ni hatua ya awali kabisa ya saratani hiyo na habari hii haikuwa mbaya sana kwa sababu saratani ikiwa katika hatua ya awali inatibika na msichana huyo anaweza kupona kabisa. Hadithi ya mgonjwa huyo inatukumbusha mambo makuu mawili; moja ni uelewa wa saratani ya mlango wa uzazi kwenye jamii zetu bado ni mdogo. Asilimia kubwa ya wanawake hawana utamaduni wa kupata vipimo mara kwa mara. Kitu pekee ninachowakumbusha wanawake na jamii kwa ujumla, saratani ya mlango wa uzazi ni miongoni mwa zinazoongoza kutishia maisha ya wanawake kuliko aina nyingine barani Afrika na sababu kubwa ni kutokana na kukosa uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo na kutopatiwa vipimo mara kwa mara.

Lakini kitu kingine, wanawake huzifumbia macho dalili zinazoashiria saratani hiyo. Mara nyingi imekua vigumu kutambua kama dalili kadha wa kadha ambazo mwanamke anazipitia zinatokana na aidha saratani au maambukizi mengine yakwenye mfumo wa uzazi. Dalili zote za saratani ya mlango wa kizazi zinafanana na zile za maambukizi ya kawaida ya kwenye mfumo wa uzazi.

Lakini mgonjwa wangu alikuwa anadhani kutokwa na hedhi iliyopitiliza na kutokwa na uchafu mwingine kumetokana na maambukizi ya kibakteria yaliyopo aidha kwenye mlango wa kizazi au ukeni hadi majibu yalipothibitisha kuwa ilikuwa ni saratani.

Usikiapo maumivu ya miguu yanayodumu, kutokwa na ute na uchafu mwingine ukeni unaotoa harufu nzito, kutokwa na damu kusiko kwa kawaida, maumivu ya kiuno na ya chini ya kitovu yasiyokoma, maumivu ya mgongo, kupungua uzito kwa kasi na uchovu uliokithiri, kamuone daktari haraka.