In Summary

Wametoa maoni hayo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha hotuba ya bajeti kuu ya Serikali bungeni mjini Dodoma jana.

Dar es Salaam. Wachumi wameichambua bajeti ya pili ya Rais John Magufuli tangu aingie madarakani, wakieleza kuwa inalenga kugusa kundi la wananchi wengi wa hali ya chini, lakini wakataka ionekane kufanya hivyo kwa vitendo.

Wametoa maoni hayo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha hotuba ya bajeti kuu ya Serikali bungeni mjini Dodoma jana.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Uchumi, Humphrey Moshi amepongeza akisema inalenga kugusa kundi la wananchi wengi wa hali ya chini, hata hivyo, akaitahadharisha Serikali kuhakikisha umuhimu wa bajeti hiyo unaonekana katika utekelezaji wake.

“Lakini pia Serikali imejifunza na kufanyia kazi malalamiko ya muda mrefu kuhusu kodi bandarini, kinachotakiwa ni utekelezaji wa hiyo bajeti maana tumeona kumekuwa na changamoto hiyo...,” alisema Profesa Moshi.

Profesa Moshi ameungwa mkono na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Dk Samweli Nyatahe aliyesema ni nzuri kwa kuwa imefanyia kazi vitu vingi vilivyokuwa vikipigiwa kelele.

Alisema angalizo lililotolewa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) la kukadiria kodi sahihi na kuachana na tabia ya kubambikiza kodi kubwa ili kuleta mazungumzo yanayosababisha rushwa nalo ni nzuri.

Kuhusu kuondolewa kwa kodi ya leseni ya magari na kuongezwa kwenye mafuta alisema itakuwa na machungu kwa mwananchi wa kawaida kwa sababu nauli za magari zitapanda lakini pia itakuwa nafuu kwa sababu malimbikizo ya tozo hiyo yalikuwa kero kwani hata gari lilipokuwa mbovu iliendelea kutozwa.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema bajeti hiyo itakuwa mwiba mchungu kwa wafanyakazi wa halmashauri baada ya kuondolewa kwa mapato yao.

Alisema itakuwa shida kwa wafanyakazi hao kwa sababu Serikali Kuu haipeleki fedha kwenye halmashauri na badala yake zinajilipa kwa mapato ya ndani.

“Ili kuwasaidia wawahamishe na malipo yao yawe kwenye namba 5004 ambayo ni ya Serikali Kuu na wawatoe kwenye namba 5000 ambayo ni ya halmashauri. Tofauti na hapo watakufa njaa labda tuone kama Serikali Kuu itapeleka fedha kwa ajili ya kuwalipa na kukwepa kuwapelekea mateso, ”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema bajeti hiyo itaongeza ushindani kwenye sekta ya viwanda kwa kuwa kuna mabadiliko makubwa ikilinganishwa na ya mwaka jana. Alifafanua kuwa kuondoa kodi katika malighafi kutasaidia kuongeza uzalishaji katika sekta ya viwanda na chakula.