In Summary

Imekuwa kawaida kwa makada wanaoishi mbali kurejea kwao kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho hasa nyakati za uchaguzi.

Dar es Salaam. Wabunge wa CCM ambao si wakazi katika majimbo yao wataisoma namba katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kueleza kwamba hawataruhusiwa kugombea kama hawaishi kwenye majimbo husika.

Imekuwa kawaida kwa makada wanaoishi mbali kurejea kwao kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho hasa nyakati za uchaguzi.

Polepole amesema hatua hiyo inatokana na chama hicho kujitathmini na kujisahihisha baada ya kugundua watu wanataka viongozi wanaotoka miongoni mwao wanaozijua na watakaoshughulikia kero zao.

Hivi sasa bado chama hicho kinaendelea na mchakato wa kuwapata viongozi wake na tayari wameshakamilisha ngazi ya wilaya kwa maeneo mengi huku, kukiwa na marufuku ya kupiga kampeni kwa namna yoyote ikiwamo matumizi ya mitandao na mabango yaliyokuwa yamezoeleka.

Akihojiwa katika kipindi cha Maisha Mseto cha Times Fm leo Alhamisi, Polepole amesema ili mwanaCCM awe na sifa za kugombea ni lazima awe mkazi wa eneo husika.

Polepole amesema suala la kuishi kwenye eneo la kugombea nafasi yoyote ya uongozi ilikuwa ni maoni ya wananchi wenyewe kwenye mchakato wa Katiba mpya.

“Shika maneno yangu 2020 wagombea wa ubunge ni wale ambao wanaotoka kwenye maeneo husika wanaojua na kushughulika na shida za wananchi,” amesisitiza.

Amesema msisitizo mkubwa ulipo ni cheo kimoja kwa mtu mmoja jambo linalofundisha kuwa watu wenye kiasi.

“Haya mambo nilikuwepo kwenye kukusanya maoni ya wananchi ndiyo watu wanayoyataka. Rais Magufuli alienda mbele zaidi kwamba utagombea nafasi ya uongozi kwenye eneo ambalo wewe ni mkazi vinginevyo, marufuku kugombea,” amesema Polepole.

Amefafanua kuwa yapo mambo ya msingi ambayo Rais Magufuli anayafanya kwenye Serikali na ndani ya chama hicho ikiwamo suala la nidhamu na namna ya kuwatumikia watu.

“Rais Magufuli anasema ukiwa kiongozi cheo ni kimoja kwa sababu mrundikano wa vyeo ni ubinafsi, CCM wameambiwa hivyo na kuna watu hawakuzoea, walizoea kuwa unaweza kuwa mbunge, mwenyekiti wa wilaya na mkuu wa wilaya mtu mmoja,” amesema na kuongeza;

 “2020 inakuja sio mtu upo zako Times Fm unapiga kazi halafu ikifika mwishoni unaenda Ileje eti unaenda kuchukua jimbo,”