In Summary
  • Anasema minyoo ni chakula bora kwa mifugo hasa kuku, kwa kuwa ina virutubisho vya protini
  • Weka kando ufugaji wa kienyeji, ambao kuku hawana ratiba ya kula, hawana viwango wala chakula maalumu kwa ajili ya ustawi wao.

Unajua kuwa ufugaji wa kisasa wa kuku, ni sayansi yenye kanuni zake maalumu?

Weka kando ufugaji wa kienyeji, ambao kuku hawana ratiba ya kula, hawana viwango wala chakula maalumu kwa ajili ya ustawi wao.

Katika ufugaji wa kisasa, sio tu kuku wanakula kwa viwango husika, lakini uchaguzi wa vyakula ni muhimu. Moja ya vyakula hivyo ni minyoo.

Unapoiogopa minyoo na hata kuitazama kwa mbali, huku ukihofu inaweza kukuambukiza magonjwa, kwa kijana Edgar Thomas, viumbe hao ni sehemu ya maisha yake.

Yeye kaamua kufuga minyooo ya rangi nyekundu kama chakula muhimu kwa mifugo hasa kuku.

Anasema minyoo ni chakula muhimu kwa kuku, kwani inawapatia virutubisho vya aina ya protini.

Tangu Januari amekuwa akijishughulisha na ufugaji wa minyoo hao anaosema ni wa asili na wala uzalishaji wake hautumii gharama nyingi, kama ilivyo katika ununuzi wa vyakula vya kemikali.

Ufugaji huu anaufanya ndani ya kibanda cha makuti na hutumia kichanja ambacho kinaanzia urefu wa mita moja.

Kwa kupitia vyombo vya plastiki ambavyo haviruhusu joto, minyoo hukua kama kawaida na huzaliana na kuvuna mingi zaidi kama mfugaji wa kawaida anayefuga mbuzi na wanyama wegine.

Ndani ya vyombo hivyo ambavyo ni ndoo na beseni, Thomas huanza kwa kuweka nyasi ambazo hazina sumu na mbolea ya ng’ombe ambayo ni kavu kama kianzio.

“Hapa inategemea kama minyoo ni kilo 10 inabidi niweke mbolea ya ng’ombe kilo tano na baada ya hapo naweka minyoo yangu juu ya mbolea kisha nachanganya na maji kwa ajili ya kuleta unyevu kisha naweka nyasi kavu juu kuzuia mwanga” anasema na kuongeza:

”Minyoo haihitaji vyakula vya gharama kwani wiki moja baada ya mchanganyiko wa majani na mbolea, hatua inayofuata ni kuwawekea mabaki ya vyakula kama vile maganda ya ndizi, matikiti, wali ambao hauna mafuta pamoja na ugali.”

INAENDELEA UK 28

INATOKA UK 27

Anasema ufugaji huu unaweza kutumiwa na mtu yeyote kwani njia zinazotumika ni za asili zisizotumia gharama kubwa.

‘’Ufugaji huu ameuona kupitia mitandao ya kijamii na hutumiwa katika mataifa mengine kama Canada, Sweden na Kenya,’’ anaeleza.

Anasema baada ya kuuona ufugaji huu, akaamua kwenda nchini Kenya kujifunza zaidi baada ya kubahatika kupata mawasiliano ya mtu aliyekuwa akifuga minyoo.

“Wengi walijiuliza juu ya minyoo kuwa chakula cha kuku wakidai ina madhara, Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha kilimo cha Jomo Kenyatta wanasema aina hii ya minyoo (Red worm) haina madhara kwa wanyama wala binadamu,”

Anasema kilichomsukuma kuanzisha mradi huu wa ufagaji wa minyoo, ni baada ya kuona wafugaji wengi wa kuku wakitumia gharama nyingi na wakati mwingine hutumia vyakula kama mahindi na mchele, ambavyo kwake ni uharibifu wa chakula.

Baada ya kuingia kwenye ufugaji, hakutaka kusumbuka aina gani ya ufugaji afanye. Fikra zake zilimsukuma kuanza ufugaji wa minyoo ambao ni maalum kwa ajili ya chakula cha kuku.

“Niliona kuwa Tanzania wanapenda ufugaji wa mazoea yaani kuku, ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine, lakini leo hii ukimweleza mtu kuhusu minyoo anaona ni kitu cha ajabu. Kwa hiyo, hii ni fursa kwangu,” anasema.

Faida ya minyoo kwa kuku

Tofauti na vyakula vingine vya kuku anasema minyoo ina asilimia 82 ya protini, ambayo humfanya kuku anenepe na kutaga mayai kwa wingi.

“Kuku anahitaji protini kwa hiyo wanapokula hii minyoo wananenepa na kutaga mayai kwa wingi. Lakini pia nitoe angalizo kuwa wapewe minyoo kulingana na kipimo, kwani wakizidishiwa kipimo, wanaweza kunenepa zaidi na kushindwa kutaga mayai” anaeleza

Thomas anayeendesha mradi wake Kivule mkoani Pwani, anasema minyoo huchukua mwezi mmoja hadi mitatu kuwa tayari na kuuza kwa wateja wake ambao ni wafugaji wa kuku na samaki.

“Kama mteja anataka minyoo, hutoa oda miezi miwili kabla ili kupunguza msongamano, kwani nisipokuwa makini naweza kuuza hadi mbegu kutokana na wingi wa wateja” anasema

Matarajio yake

Thomas hajatosheka wala hajafika mwisho wa safari yake. kwanza anatamani kuwa na mradi mkubwa wa ufugaji wa minyoo ili aweze kuzalisha idadi kubwa kuliko ilivyo sasa.

Anapenda kuwa mzalishaji mkubwa wa minyoo Afrika Mashariki na Kati pamoja na kutoa elimu kwa anayetaka kujua jinsi ya kufuga minyoo

‘’ Nina lengo la kuonana na Serikali hasa idara ya mazingira niweze kuingia ubia kwa kushika tenda za kukusanya taka katika masoko mbalimbali, kwani minyoo inatumia zaidi taka zitokanazo na mabaki ya vyakula na matunda,’’ anasema na kuongeza kuwa lengo lake kwa baadaye ni kutoa ajira kwa watu zaidi ya 150 hasa vijana wasiokuwa na kazi.

Ufugaji ni fursa

Anasema tangu agundue fursa kwenye ufugaji, ameamua kujikita rasmi kama mfugaji na hajali kuwa mfugaji wa minyoo japo kwa taaluma yake ya sheria angeweza kutafuta ajira kama zilivyo fikra za vijana wengi wa Kitanzania, wanaoamini msomi hawezi kujiajiri hasa katika sekta kama ufugaji tena huu wake wa minyoo ambayo kwa wengi ni sawa na karaha.

Anaamini kuwa endapo Watanzania watakuwa makini katika ufugaji na kuwa tayari kujifunza na kuacha ufugaji wa kimazoea, sekta hiyo inaweza kuwatoa wengi kutoka katika umasikini.

“Ufugaji unaweza kumletea faida mfugaji lakini atafanikisha haya kama atakuwa na jitihada na maarifa hasa katika masoko,”anaongeza.

Changamoto

Thomas anasema changamoto ambayo anakumbana nayo katika ufugaji wake ni upatikanaji wa mbegu ya minyoo aina ya Red worm.

“Kwa hapa nchini kama unahitaji mbegu kuanzia kilo 50 huwezi kupata, kwa kuwa bado hatujapata wafugaji wakubwa wanaoweza kuzalisha minyoo mingi,”anasema na kuongeza:

‘’ Marafiki na jamaa wanaona kuwa kufuga minyoo ni kuhatarisha afya yangu kwa kuchezea uchafu, hali inayofanya nirudi nyuma kwa kuona kuwa nadharaulika”

Anatoa rai kwa Serikali kutoa msaada kwa wananchi ambao wameamua kutumia nguvu na maarifa yao kuwekeza kwenye ufugaji huu ambao hauna hasara.

“Ufugaji wa aina hii unahitaji kuungwa mkono na Serikali na watu wanapaswa kutambua mengi zaidi juu ya ufugaji wa minyoo. Nafahamu kuwa wapo wataalamu katika masuala ya ufugaji lakini tupo na sisi ambao tumejiongeza,” anasema Thomas ambaye pia analima matunda na mchaichai.

Anasema mradi huu kama utapewa kipaumbele, una uwezo wa kusaidia zaidi ya vijana 200 kupata ajira na kuondokana na wimbi kubwa la utegemezi.