In Summary

Kupitia mitandao hiyo, wanasiasa pia wametumia fursa hiyo kutuma ujumbe mbalimbali kuwasiliana na wafuasi wao, huku kwa siku za karibuni viongozi wa kitaifa na Jeshi la Polisi wakijitokeza kujibu hoja zinazoibuliwa mitandao.

Dar es Salaam. Mabadiliko ya kidunia kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano, yamekuwa chanzo cha Watanzania wengi kubadili utamaduni wa kupashana habari na kwa kiwango kikubwa kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa kupitia mitandao ya kijamii.

Kupitia mitandao hiyo, wanasiasa pia wametumia fursa hiyo kutuma ujumbe mbalimbali kuwasiliana na wafuasi wao, huku kwa siku za karibuni viongozi wa kitaifa na Jeshi la Polisi wakijitokeza kujibu hoja zinazoibuliwa mitandao.

Suala la karibuni zaidi kutikisa kupitia mitandao ya kijamii ni la uhamasishaji wa maandamano Aprili 26, ambayo tayari yamepigwa marufuku na Serikali.

Baadhi ya mitandao hiyo ambayo imeunganisha mamilioni ya watu ni Facebook, Twitter, YouTube, WhatsApp na Instagram, ambayo inaelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa inatumika zaidi kwa shughuli za siasa.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Februari, inaonyesha kuwa Tanzania inakua kwa kasi katika matumizi ya intaneti baada ya kufikisha watumiaji zaidi ya milioni 23 mwaka 2017, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya watumiaji wa miaka mitano iliyopita.

Katika watumiaji hao waliorekodiwa mwaka jana, wanane kwa 10 wanatumia intaneti inayohamishika, ambayo hutumika zaidi katika simu za mkononi, tablet na kompyuta mpakato (laptop).

Wadadisi wa masuala ya Tehama walisema sababu zinazochagiza mwamko huo, ni maendeleo ya teknolojia hiyo, uharaka na gharama nafuu tofauti na njia nyingine za kupashana habari.

Mhadhiri msaidizi katika Idara ya Mawasiliano kwa Umma, Chuo Kikuu cha Tumaini, tawi la Dar es Salaam (Tudarco), Richard Ngaiza anasema ongezeko ni kubwa na uhuru wa watu kujieleza umeongezeka zaidi katika mijadala ya kisiasa. “Sababu za mwamko mkubwa ni kutokana na uharaka wa kuwasiliana, inaokoa muda ukilinganisha na njia nyingine, lakini mwamko umeongezeka kwenye mijadala ya kisiasa baada ya watu kubanwa katika njia nyingine za kushiriki kama vile majukwaa ya hadhara, wanapata sehemu ya kupumulia,” alisema.

Ngaiza anaungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia, Elimu na Menejimenti katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Edephone Mfuka aliyesema kuwa ongezeko la watu katika mitandao ya kijamii ni mafanikio kwa taifa na tafiti nyingi zimekuwa zikihamasisha huduma za kijamii kuhamia huko.

“Sasa kuna wanaoingia kwa nia njema na nia mbaya. Hii inaonekana katika mataifa mengi duniani. Mitandao hiyo imewekewa mifumo ya kufuatilia tabia za watumiaji wake, kuna uwezekano wa kudhibiti wanaoingia na kufuatilia waliopo ndani ya mitandao hiyo,” alisema Dk Mfuka akishauri Watanzania kuitumia kwa manufaa ya kiuchumi, kuongeza uzalishaji na maarifa na kuepuka habari za upotoshaji.

Akijadili suala hilo, Profesa Mohammed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kuhusu kundi la watumiaji wa masuala ya kisasa limekuwa na faida kubwa kuliko hasara.

Alisema mitandao hiyo imekuwa jukwaa linalokuza kiwango cha uhuru wa kujieleza katika nchi zinazoendesha mfumo wa kidemokrasia. “Muhimu ni kuepuka habari za upotoshaji lakini jamii inanufaika nayo zaidi, kwa sababu majukwaa mengine ya kushiriki siasa yamebanwa, kwa mfano, mikutano ya hadhara,” alisema.

Mmiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg Julai mwaka jana alitangaza mtandao huo kufikisha watumiaji bilioni mbili kwa mwezi. WhatsApp ina watumiaji zaidi ya bilioni moja duniani wakati Instagram inatajwa na mtandao wa unaojihusisha na ukusanyaji wa takwimu za watumiaji wa mitandao, ‘Statista’, kuwa na watumiaji milioni 800 kwa mwezi.

Matumizi ya mitandao

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Luqman Maloto anasema sehemu kubwa ya maudhui ya falsafa ya siasa na teknolojia katika dunia ya sasa inabebwa na simu za mkononi.

Hata hivyo, anasema wanasiasa wengi nchini hawakujitayarisha kwa ajili ya mabadiliko hayo, isipokuwa wamezolewa tu na mkumbo wa mapinduzi ya kiteknolojia.

Katika andiko lake la hivi karibuni kwenye gazeti hili, Maloto anasema teknolojia inarahisisha mipango ya kisiasa bila mikutano ya hadhara, akitolea mfano Tundu Lissu akiwa kitandani hospitalini Nairobi, Kenya na baadaye Ubelgiji, anavyozungumza na Taifa na ujumbe unavyoenea kila mahali.

“Anajirekodi akiwa hospitali, sauti inaingizwa YouTube. Watu wanachukua sauti yake YouTube na kuipeleka Facebook na makundi ya WhatsApp, vilevile inakatwa nusunusu na kuwekwa Twitter na Instagram. Sauti inafika kwa wapigakura wake na kila eneo, kisha inajadiliwa kwenye majukwaa mbalimbali,” alisema Maloto.

Pili, alisema kuna mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, Facebook Live, Instagram Live na YouTube Live ambao umewezesha kufanya mikutano bila kuhitaji waandishi wa habari, bali kwa ulimwengu mzima.

Alisema hatua hiyo ni mapinduzi makubwa ya kiteknolojia ambayo yanafanya siasa za majukwaa ya kawaida zianze kupitwa na wakati.

Kwa hapa nchini, mtandao wa Socialbakers, unataja wanasiasa sita kati ya watu 20 wenye wafuasi wengi kuliko Watanzania wote wanaotumia Twitter.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete anaongoza kwa kuwa na wafuasi 1,000,030 akifuatiwa na Zitto Kabwe (720,000), Halima Mdee (502,716), Januari Makamba (489,804), Rais John Magufuli (397,637) na Profesa Jay (341,871).