In Summary
  • Mbunge Mtwara Vijijini ajitolea mifuko 100 ya saruji

Mtwara. Wakazi wa kijiji cha Mtendachi halmashauri ya wilaya Mtwara wamejitolea kujenga shule ya msingi kijijini hapo ili kuwaondolea watoto wao adha ya kutembea umbali mrefu  kwenda shule iliyopo kijiji jirani cha Nomindondi.

Uamuzi huo umekuja baada ya shule iliyokuwepo kijijini hapo kuharibiwa na mafuriko mwaka 1984.

Mwananchi leo Januari 14, 2018 limeshuhudia wakazi hao wakisomba mchanga na kubeba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwa ni baada ya kukubaliana kufanya ujenzi huo katika mkutano wa kijiji uliofanyika mwaka jana.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Salum Muhidin amesema, “ Nimekuwa nikiwahamasisha  wananchi kuhusu jambo hili kwa sababu watoto wao wanatembea umbali mrefu. Naomba wadau mbalimbali watuunge mkono ili mwisho wa mwezi ujao watoto waanze kutumia majengo ya shule.”

Amesema baada ya ujenzi huo kukamilika shule hiyo itaitwa Mikumba.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kijiji hicho kina wakazi 1,971 lakini hakina shule ya msingi tangu mwaka 1984 baada ya shule iliyokuwepo kuharibiwa na mvua.

"Tangu mwaka 1984, watoto wetu wanasoma shule ya kijiji jirani cha Nomindondi. Tumeazimia kuondokana na aibu hii kupitia mkutano mkuu wa kijiji uliofanyika mwaka jana kwa kukubaliana  kujenga shule kwa nguvu zetu,” amesema Muhidini.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Adinani Said amesema baada ya shule hiyo kuharibiwa na maji, wazee wakati huo waligoma kutoa maeneo ya mashamba yao kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Akizungumzia juhudi hizo, mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia ametoa mchango wa mifuko 100 ya saruji.

Halmashauri ya wilaya ya Mtwara yenye wakazi zaidi ya 134, 530 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, ina shule 67 za msingi na 11 za sekondari za umma. Halmashauri hiyo ina vijiji 110 na kata 21.