In Summary

Kuanzia Novemba Mosi mpaka 10, wateja 20 wa shirika hilo wanaweza kushinda tiketi za daraja la tatu (economy class) na la pili (business class) zenye punguzo hilo ambazo wanaweza wakatumia kati ya Novemba Mosi mpaka Oktoba 31 mwakani.

Dar es Salaam. Likisherehekea miaka 20 ya huduma, Shirika la Ndege la Qatar limetangaza punguzo la bei kwa tiketi zitakazodumu kwa mwaka mzima.

Kuanzia Novemba Mosi mpaka 10, wateja 20 wa shirika hilo wanaweza kushinda tiketi za daraja la tatu (economy class) na la pili (business class) zenye punguzo hilo ambazo wanaweza wakatumia kati ya Novemba Mosi mpaka Oktoba 31 mwakani.

Ofisa mkuu wa biashara wa shirika hilo, Ehab Amin alisema kwenye promosheni hiyo, abiria wa business class anaweza kushinda tiketi mbili akilipia moja wakati wa economy akipata tatu akilipia mbili.

“Huu ni mwaka maalumu wa kuwaleta karibu wateja wetu kuwashirikisha kwenye maadhimisho haya muhimu. Abiria wetu kutoka popote duniani wanaweza kushiriki shindano hili wanapoandaa safari zao kuelekea watakako kati ya vituo vyetu 150 vilivyopo,” alisema ofisa huyo.

Licha ya tiketi hizo zenye punguzo la mpaka asilimia 50, abiria wa Qatar iliyopata tuzo ya shirika bora la ndege zinazotolewa na Skytrax mwaka huu, wanaweza kujishindia uanachama wa wateja maalumu (Privilege Club Gold) waliosambaa duniani kote.

Mwaka huu pekee, shirika hilo linalokuwa kwa kasi lenye zaidi ya ndege 200 zimeanza kutua Auckland (New Zealand), Dublin (Ireland), Nice (Ufaransa) na Prague (Jamuhuri ya Czech) huku ikipanga kufanya hivyo Canberra (Australia), St. Petersburg (Urusi) na Cardiff (Uingereza) mwakani.