In Summary

Fedha hizo zimetolewa baada ya wanafunzi 52 wa shule za sekondari na msingi wilayani hapa kukatisha masomo kutokana na ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Nyang’hwale. Serikali wilayani hapa imetoa Sh150 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni matano kwenye Shule ya Sekondari Msalala mkoani Geita.

Fedha hizo zimetolewa baada ya wanafunzi 52 wa shule za sekondari na msingi wilayani hapa kukatisha masomo kutokana na ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Hivyo, ujenzi huo ni miongoni mwa njia za kupambana na mimba shuleni kwa kuwa wanafunzi wataepuka kutembea umbali mrefu.

Akizungumza wakati wa kutoa tathmini ya mafanikio wilayani hapa kwa mwaka uliopita, mkuu wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyama alisema tatizo la mimba limekuwa moja ya changamoto zinazokatisha ndoto za wanafunzi hao.

Gwiyama alisema moja ya mikakati muhimu mwaka 2018 ni kutatua changamoto hiyo kwa kujenga mabweni ili kuwasaidia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kuondokana na vishawishi wanavyokutana navyo njiani.

“Serikali imeamua kutatua changamoto hiyo, tayari imejenga mabweni katika shule za sekondari Kakola na Busolwa kwa fedha ambazo zimetokana na mapato ya ndani na nguvu za wananchi.

“Serikali imewaunga mkono wananchi kwa kutoa kiwango hicho cha fedha kufanikisha ujenzi wa mabweni matano katika Shule ya Msalala,” alisema Gwiyama.

Alifafanua kuwa pamoja na tatizo la mimba kuwa doa katika sekta ya elimu, kiwango cha elimu kinazidi kukua na mwamko wa elimu kwa wananchi unaongezeka.

Alisema wilaya ililenga kuandikisha wanafunzi 4,417 darasa la kwanza lakini hadi sasa wameandikisha 13,247 ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya lengo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Msalala, David Obadia alisema umaskini, mila potofu na umbali ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanafunzi kupata mimba katika shule hiyo.

Alisema kwa kipindi cha mwaka 2016/17 wanafunzi zaidi ya 17 waliacha masomo kwa kupata mimba.

Obadia alisema wao kama walimu wanajitahidi kuzungumza na wanafunzi na wazazi kuhusu madhara ya mimba za utotoni.

Alisema kati ya wanafunzi 400 wa shule hiyo walioripoti shuleni hadi sasa ni 90 na wengi wao wanadai wameshindwa kufika kwa kukosa madaftari na nguo za shule.

Ofisa elimu wa wilaya hiyo, Daines Mosha alisema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kutokomeza mimba mashuleni bado baadhi ya watendaji ngazi ya chini wamefanya mimba kuwa ‘dili’ ya kujipatia kipato.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Geita, Rehema Mbwiro alisema wanafunzi 218 wa shule za msingi na sekondari walikatisha masomo kati ya mwaka 2013 na 2017 baada ya kupata ujauzito.