In Summary

Ulinzi utaimarishwa kwa kutumia kamera maalumu kubaini kila anachofanya mtu ndani ya jengo hilo.

Dar es Salaam. Jengo jipya la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), litakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 6.5 milioni kwa mwaka baada ya kukamilika.

Idadi hiyo ni mara nne zaidi ya jengo la abiria namba mbili (Terminal II) ambalo linahudumia abiria 1.5 milioni kwa mwaka.

Ujenzi huo umefikia asilimia 67 na unatarajiwa kukamilika mapema mwakani.

Gharama za jumla kwa ujenzi wa jengo hilo ni Sh560 bilioni na Serikali imeazimia kukamilisha ujenzi mapema baada ya kusimamishwa kwa muda kutokana na uhaba wa fedha za kumlipa mkandarasi, kampuni ya BAM kutoka Uholanzi.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo leo Alhamisi Desemba 7,2017 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege nyingi kwa wakati mmoja.

Amesema litahudumia ndege kubwa 11 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 300 na 400; ndege za kati 21 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 120 na 160 kwa wakati mmoja.

Ili kukabiliana na msongamano wa abiria ambao wanachukua muda mrefu kupata huduma, Profesa Mbarawa amesema jengo hilo litakuwa na maofisa uhamiaji 24 ambao watafanya kazi kwa haraka na kupunguza foleni katika jengo hilo.

"Jengo hili likikamilika, abiria hatatumia zaidi ya dakika 15 au 20 baada ya kushuka. Kila mtu anapenda akishuka kwenye ndege awahi kwenda nyumbani na si kutumia muda mrefu uwanja wa ndege," amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Richard Mayongela amesema jengo la abiria namba tatu litakuwa na mitambo ya kisasa ya usalama kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Amesema watafunga kamera za CCTV kwenye jengo hilo ili kumfuatilia kila mtu na kubaini anachofanya ndani ya jengo hilo, pia kuchukua hatua ikibainika kwamba mtu huyo anahatarisha usalama ndani ya jengo.

"Serikali imeunda timu maalumu ya kuhakikisha kwamba mitambo yote ya kiusalama inaunganishwa ili kulitazama jengo lote kila kona," amesema.