In Summary

Serikali imesaini mkopo nafuu na  Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kufungua utalii kwenye mikoa ya Kusini ili nayo ichangie kwenye Pato la Taifa.

Dar es Salaam. Serikali imesaini mkataba wa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) wenye thamani ya Sh340 bilioni kwa ajili ya kufungua utalii kwenye mikoa ya Kusini ili nayo ichangie kwenye Pato la Taifa.

Mradi huo unalenga kuufanya mkoa wa Iringa kuwa kitovu cha utalii katika ukanda huo na utaambatana na uboreshaji wa miundombinu, kuvutia utalii na kuibua fursa nyingine za kiuchumi ili wananchi wanufaike na sekta hiyo.

Mkataba huo umesainiwa leo Novemba 8 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird na kushuhudiwa pia na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi.

Akizungumzia mkopo huo, James amesema ukanda wa Kusini una vivutio vingi lakini mchango wake umekuwa mdogo kwa sababu watalii wengi hawaendi kutokana na miundombinu duni na kutotangazwa vya kutosha.

Amesema mkopo huo utasaidia kuimarisha hifadhi za Kusini ikianzia na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya ile ya Etosha inayopatikana Namibia.

“Mradi huu utaenda mpaka hifadhi nyingine za Kusini ikiwemo Mikumi na Selous na shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kujenga madaraja na uwanja wa ndege wa Iringa. Wananchi watapata fursa nyingi za kiuchumi kupitia mradi huu,” amesema James.

Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa watajenga pia barabara ya kiwango cha lami kuunganisha mji wa Iringa na Hifadhi ya Ruaha bila kuathiri mazingira. Amesema barabara hiyo itaongeza idadi ya watalii watakaotembelea hifadhi ya Ruaha.

Kuhusu kuongezeka kwa deni la Taifa kutokana na mikopo hiyo, James amesema deni la Taifa bado ni stahimilivu ndiyo maana WB imeikopesha Tanzania. Amefafanua kwamba taarifa za kwamba deni la Taifa limepaa siyo za kweli kwa sababu bado haijafikia ukomo.

“Ukomo wa deni la Taifa ni asilimia 50, sisi tumefikia asilimia 32, kwa hiyo bado tuna ziada ya kukopa tena ya asilimia 18. Nchi inakopesheka vizuri na tunaweza kwenda kukopa tena kama tunataka.”

“Mimi ndiye mtunza fedha, hali ninaijua. Kwa hiyo mkawaelimishe hao wanaopotosha kwamba deni linapaa,” amefafanua kiongozi huyo wakati wa kutiliana saini mkopo mwingine wa Dola za Marekani 150 milioni (Sh340 bilioni).

Kwa upande wake, Bella Bird amesema suala la utunzaji wa mazingira na maliasili ni vipaumbele kwa pande zote mbili ndiyo maana WB iliidhinisha mkopo huo Septemba 28 mwaka huu ili ukafanye kazi iliyokusudiwa.

Amesema utalii unafanya mambo mengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi kutokana na ajira zinazotengenezwa, kutunza mazingira na kuhifadhi ikolojia ya viumbe kwenye hifadhi hizo.

Amebainisha kwamba shughuli zinazokwenda kufanyika lazima zilenge kuleta maendeleo na maendeleo ni kwa ajili ya watu. Amesisitiza kwamba wakati mwingine utunzaji unaathiri maisha ya watu.

“Mradi wa Iringa unaweza kuwa mfano wa kuigwa ulimwenguni, mambo mengi yatafanyika katika mradi huo ambao utatoa fursa za kiuchumi na kuhifadhi mazingira,” amesema mkurugenzi huyo wa WB.