In Summary

Ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua  ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma, eneo la Makutopora


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema wananchi kulipa kodi isiwe kero kwao, bali heshima na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa makini.

Akizungumza leo Machi 14, 2018 mjini eneo la Ihumwa nje kidogo ya Mkoa wa Dodoma wakati akizindua ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutopora, Rais Magufuli amesema baadhi ya kodi wananchi hukwepa kulipa kodi kutokana na namna zinavyotozwa na viwango kuwa juu.

“Kuna watu TRA siyo wazuri, Kamishna wa TRA na Waziri wa Fedha  shughulikieni hili. Mtu kulipa kodi isiwe ni kero bali heshima,” ameagiza.

Kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli amesema katika awamu zote za ujenzi itagharimu Sh15 trilioni.

“Ukiachilia mbali mradi huu, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya miundombinu. Hapa Dodoma tunajenga barabara za mizungumko, kazi ya designing (usanifu) inafanyika na itakuwa kwa kiwango cha lami ili kweli Dodoma ionekane makao makuu ya nchi,” amesema.