In Summary

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema utekelezaji  unapaswa kufanyika ndani ya siku 90 kuanzia leo Novemba 8,2017.

Dar es Salaam. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema nyumba za wakazi wa Mnyamani- Buguruni jijini Dar es Salaam zilibomolewa kimakosa pasipo sheria na utaratibu kufuatwa.

Tume pia imetoa siku 90 kwa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kuwalipa fidia wananchi hao, huku ikilitaka Jeshi la Polisi kuacha kusimamia uvunjifu wa amani pale wananchi wanapodai haki zao.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga amesema hayo leo Jumatano Novemba 8,2017  alipotoa uamuzi wa shauri la wakazi hao wanaopinga nyumba zao kubomolewa na Rahco.

Amesema walalamikiwa katika shauri hilo ni Said Bindo na wenzake 72 dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, M/S Hepautwa Investment and General Brokers Ltd na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).

Nyanduga amesema kwa mujibu wa sheria, Dar es Salaam hakuna vijiji bali kote ni mjini na mita kutoka katikati ya reli ni 15 na si 30 kama ambavyo Rahco ilibomoa nyumba za Mnyamani ikijua kufanya hivyo inakiuka sheria za nchi.

"Ubomoaji wa nyumba katika eneo la mita 30 eneo la Mnyamani haukuwa halali. Ni dhahiri kwamba waliovunjiwa nyumba wanastahili kulipwa fidia, kwa kuwa ni haki yao ya msingi inayotambuliwa na Katiba ya nchi Ibara ya 24(2) na sheria za nchi," amesema Nyanduga.

"Utekelezaji huu unapaswa kufanyika ndani ya siku 90 kuanzia leo Novemba 8,2017 na mapendekezo yote tutayawasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya utekelezaji," amesema.

Nyanduga amesema haikuwa haki kwenda kubomoa nyumba hizo saa 11:00 alfajiri kwa kuwa kulikuwa na wagonjwa, watoto, wazee ambao bado walikuwa wamelala, hivyo walikiuka misingi ya haki za binadamu za kuheshimiwa na kupewa makazi.

Ubomoaji huo uliofanyika Machi 11 hadi 13,2017, imeelezwa na Nyanduga kwamba ulisababisha uharibifu wa mali.

Amesema Jeshi la Polisi lililopaswa kulinda amani halikufanya hivyo, huku mabaunsa waliotumika hawakupaswa kuwepo eneo hilo.

Mwakilishi wa wananchi hao, Msafiri Bonamali amesema uamuzi uliotolewa unabidi kutekelezwa na walipwe fidia kutokana na kubomolewa kimakosa nyumba zao.

Ofisa Sheria wa Rahco, Pamela Swai amesema watachukua mapendekezo hayo na kwenda kuyapitia katika kikao cha menejimenti.