Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo na inatarajia kumfikisha mahakamani, kwa kile ilichodai kuwa alidanganya kwamba ametekwa.

Nondo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alidaiwa kutoweka usiku wa Machi 6 mwaka huu na baadaye alipatikana Mafinga, Iringa na kujisalimisha polisi akidai kwamba alitekwa.

Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema jana kuwa atafikishwa kortini baada ya upelelezi kukamilika ili akajibu mashtaka matatu; kudanganya, kusababisha taharuki kwa wanafunzi na usumbufu kwa uongozi wa chuo hicho cha umma.

“Tumebaini kuwa Nondo hakutekwa, bali alijiteka mwenyewe. Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa alikuwa anawasiliana na mpenzi wake mara kwa mara akiwa njiani kuelekea mkoani Iringa,” alisema Mambosasa.

Itakumbukwa kuwa Kamanda wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire aliwaeleza wanahabari kuwa walifungua jalada la uchunguzi ili kubaini iwapo kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani.

Wakati bado akiwa Iringa, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alilitaka jeshi hilo kumrejesha mkoani mwake litakapomaliza uchunguzi ili ufanyike mwingine kubaini iwapo alijiteka au la.

Jana, Mambosasa alisema kwa kushirikiana na polisi Mkoa wa Iringa, walifanya uchunguzi na kubaini kuwa mwanafunzi huyo hakutekwa, bali alijiteka mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kuzua tafrani kwa jamii.

Alisema Machi 6 saa sita usiku zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana.

Alisema walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo ikiwa pamoja na kufunguliwa jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.

Mambosasa alisema Machi 7, walipata taarifa kutoka polisi Iringa kuwa mwanafunzi huyo ameonekana wilayani Mufindi mjini Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua anaendelea na shughuli zake.

“Mwanafunzi huyu alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa katika kituo chochote cha polisi. Ndiyo maana tunaendelea kumshilikia ili taratibu zikikamilika tumpeleke mahakamani,” alisema Mambosasa.

Mambosasa alisema baada ya kuchunguza kitaalamu mawasiliano ya simu yake kwa kipindi chote ‘alichojiteka’ na hata baada ya kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alipimwa na kubainika kuwa hakupewa aina yoyote ya kinywaji au dawa za kumpoteza fahamu na alionekana ni mtu mwenye afya njema hana majeraha ya aina yeyote katika mwili mwake.