In Summary

Watuhumiwa waliiambia mahakama kwamba walikamatwa walipokuwa majumbani kwao na wakawekwa kizuizini kinyume cha sheria katika mahabusu za kijeshi kabla ya kusafirishwa hadi Kituo cha Polisi cha Nalufenya wilayani Jinja ambacho ni maarufu kwa kuendesha mateso.

 

Kampala, Uganda. Mahakama Kuu imeiamuru Serikali ya Uganda kuwalipa fidia ya zaidi ya Sh1,760,000,000 watahumiwa 22 wa mauaji ya aliyekuwa msemaji wa polisi Andrew Felix Kaweesi kwa kuvunjiwa haki zao za msingi walipokuwa mahabusu.

Hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa jana na Jaji Margret Oguli inataka kila mtuhumiwa kulipwa fidia ya Sh80 milioni za Uganda.

Jaji Oguli amesema kwamba serikali inapaswa kulipa kiasi hicho pamoja na riba ya asilimia 20 kuanzia siku ilipotolewa hukumu (Oktoba 12, 2017) kwa maelezo kwamba mamlaka za magereza zilikiuka haki zao kwa kuwatesa watuhumiwa hao walipokuwa mahabusu.

“Walalamikaji bado ni watuhumiwa tu hadi mahakama itakapothibitisha kuwa wana hatia. Hivyo basi, wanapaswa kutendewa vizuri bila mateso,” amesema.

Kwa mujibu wa jaji huyo, kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa mamlaka za magereza zilikuwa zinaficha kitu fulani pale walipotakiwa kuwapeleka watuhumiwa hao wakapate matibabu.

Hukumu hiyo imekuja baada ya mwanasheria wa watuhumiwa Ladislaus Rwakafuzi kuomba mahakama iilazimishe serikali kuwapeleka watu hao hospitalini wakachunguzwe ili kujua chanzo cha majeraha waliyokuwa nayo.

Watuhumiwa waliiambia mahakama kwamba walikamatwa walipokuwa majumbani kwao na wakawekwa kizuizini kinyume cha sheria katika mahabusu za kijeshi kabla ya kusafirishwa hadi Kituo cha Polisi cha Nalufenya wilayani Jinja ambacho ni maarufu kwa kuendesha mateso.

Vilevile waliiambia mahakama kwamba hawakupewa matibabu kwa ajili ya kuponya vidonda vilivyokuwa vinanuka usaha.

Kaweesi aliuawa kwa kupigwa risasi pamoja na mlinzi wake binafsi na dereva wake Machi 17 mwaka huu wakati akiondoka nyumbani kwake Kulambiro. Watu kadhaa walikamatwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo na wakawekwa mahabusu lakini baadaye wengi wao walionekana wakiwa na vidonga walivyodai vilitokana na mateso makali waliyopata kutoka kwa maofisa wa usalama.