In Summary
  • Taasisi za umma zashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima

Chama cha Makandarasi Wazalendo Tanzania (ACCT), kimeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuzielimisha taasisi za umma kutumia dhamana za bima badala ya kung’ang’ania za benki wanapotoa kazi kwa kampuni za ukandarasi.

Mwenyekiti wa ACCT, Mhandisi Milton Nyerere alisema jana kuwa matumizi ya dhamana za bima zitatoa urahisi kwa kampuni kutekeleza majukumu yake.

Alisema hivi sasa taasisi za Serikali zimekuwa zikizilazimisha kampuni zinazoshinda zabuni kuweka dhamana za benki na kuzikataa za kampuni za bima.

Alisema Sheria ya Manunuzi ya Umma inazitaka taasisi za umma kuomba dhamana za aina mbili za benki na za kampuni za bima.

“Imezoeleka taasisi za umma zinapotoa zabuni kwa wakandarasi zinataka dhamana za benki.

“Hazitaki za kampuni za bima, hiki ni kikwazo kwetu makandarasi wazalendo,” alisema Nyerere.

Akifafanua kuhusu changamoto za dhamana ya benki, Nyerere alisema sheria inataka kampuni iliyoshinda zabuni kumpa mteja wake dhamana ya asilimia 10 ili kumkinga iwapo kutatokea uzembe katika utekelezaji wa mradi.

“Hii ina maana kama mkandarasi atapewa atekeleze mradi wa Sh1 bilioni; atatakiwa kuweka dhamana benki ya asilimia 10.

“Kampuni zetu za kizalendo tutapata wapi dhamana ya nyumba za thamani hiyo katika kila mradi tunaoutekeleza,” alisema Nyerere.

Pia, alisema wakati umefika kwa taasisi za umma kuwapa makandarasi uwezo wa kuchagua ni dhamana ipi wanataka kuiweka ili waweze kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.

Alishauri taasisi za umma kuwasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (Tira) ili kampuni za bima ziweze kushiriki kuwa wadhamini wa kampuni za ukandarasi.

Nyerere alidai kuwa kitendo cha taasisi za umma kuzikataa dhamana za bima huenda wanatumiwa na kampuni za makandarasi za kigeni ili kuwatoa wazalendo kwenye sekta ya ujenzi.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PPRA, Mcharo Mrutu alisema kazi ya mamlaka hiyo ni kusimamia Sheria za Manunuzi ya Umma iliyopo.

Mrutu pia alisema sheria inaziruhusu taasisi za umma kudai dhamana za kampuni za bima au za benki.

Pia, alishauri chama hicho kupeleka maoni yao kwenye Idara ya Sera ya Manunuzi ya Umma iliyopo Wizara ya Fedha na Uchumi ili kuingalia upya sheria hiyo.