In Summary
  • Pia ametaka iwasimamie makandarasi hao kwa karibu ili kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inalingana na kiasi cha fedha wanacholipwa.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati ijiridhishe na ubora wa vifaa vinavyotumiwa na makandarasi katika miradi ya umeme.

Pia ametaka iwasimamie makandarasi hao kwa karibu ili kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inalingana na kiasi cha fedha wanacholipwa.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika kikao cha maendeleo ya usambazaji umeme kilichofanyika, ofisini kwake, Dodoma.

Alisema wakati huu ambao Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) wakiendelea na miradi ya usambazaji umeme, ni vyema wizara hiyo ikajiridhisha na ubora wa vifaa.

“Wasimamieni makandarasi kikamilifu na kama hamjaridhishwa na kazi wanayofanya msisite kuwachukulia hatua, tunataka wananchi wapate umeme.”

Alisema Rais John Magufuli amedhamiria kuona umeme unasambazwa kwenye vijiji vyote nchini kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi.

Alisisiza kwamba ni lazima makandarasi waliopewa jukumu hilo wasimamiwe kikamilifu ili mradi hiyo iweze kuwa na ubora unaostahili.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema tayari makandarasi wanaotekeleza mradi wa Rea namba tatu wameshaanza kazi.

Alisema kwa makandarasi ambao bado hawajaanza, wamekubaliana kwamba wataanza wakati wowote na wa mwisho ataanza Machi 2.

Dk Kalemani alisema wizara yake itahakikisha miradi yote ya kusambaza umeme inasimamiwa kikamilifu na inakamilika kwa wakati na katika ubora unaostahili.