In Summary

Musukuma ameondoka huku akiwataka wanaCCM wilayani Geita kuacha majungu na makundi iwapo wanataka kulinda jimbo hilo uchaguzi mkuu wa 2020

Geita. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita aliyemaliza muda wake, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ ameondoka huku akiwataka wana CCM wilayani Geita kuacha majungu na makundi iwapo wanataka kulinda jimbo hilo uchaguzi mkuu wa 2020.

Akihutubia mkutano mkuu wa uchaguzi wa mkoa huo uliomweka madarakani Alhaji Said Kalidushi kwa ushindi wa 358, kati ya 666 zilizopigwa, Musukuma alisema chama hicho kinajua uwepo wa fitina na majungu miongoni mwa wana CCM wanaopanga njama za kumng’oa mbunge wa sasa wa jimbo la Geita, Costantin Kanyasu uchaguzi ujao kwa kumkwamisha kutekeleza ahadi na majukumu yake ya kibunge.

“Wana CCM jimbo la Geita watengeneza makundi ya kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020; chama hakitakubali mgawanyiko utakaotufanya tupoteze jimbo 2020,” Musukuma

Aliwaasa wajumbe wa mkutano huo kumchagua mtu atakayekuwa na uthubutu wa kusema hapana kwa makundi ya chuki, fitina na majungu ndani ya chama ili kukivusha salama kwenye chaguzi za serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.