In Summary

Alisema lengo la kusambaza ujumbe huo ilikuwa ni mikakati ya wanasiasa kuharibu utendaji wake wa kazi ikiwamo kuvuruga mkutano wa hadhara aliokuwa amepanga kuufanya siku hiyo.

Dar es Salaam. Sakata la kuzushiwa kifo Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema limechukua sura mpya baada ya kiongozi huyo kutaka waliosambaza taarifa hizo wamlipe fidia ya Sh20 bilioni kutokana na usumbufu alioupata.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Parole alisema hayo jana mara baada ya kufika Kituo cha Polisi Osterbay kutoa taarifa za uzushi huo aliodai umemsababishia usumbufu yeye, ndugu zake na watoto wake.

Januari 9, katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zilisambaa taarifa za kufariki dunia kwa mwanasiasa huyo mkongwe nchini katika Hospitali ya KCMC- Moshi mkoani Kilimanjaro.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha Polisi Osterbay, Mrema alisema ametoa taarifa kituoni hapo na kupewa RB namba OB/NB/613/2018 ya matumizi mabaya ya mtandao.

Alisema lengo la kusambaza ujumbe huo ilikuwa ni mikakati ya wanasiasa kuharibu utendaji wake wa kazi ikiwamo kuvuruga mkutano wa hadhara aliokuwa amepanga kuufanya siku hiyo.

Alisema kutokana na uzushi huo, ametoa taarifa Mamlaka kwa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambako alitakiwa kutoa taarifa polisi.

“Ndio maana leo (jana) hii nimekuja kutoa taarifa hapa polisi na wamenieleza wanalifanyia kazi na watakaobainika watafunguliwa kesi na nitadai fidia ya Sh20 bilioni ya usumbufu na kunichafua kwenye mitandao,” alisema Mrema.

“Siku hiyo nilipanga nifanye misa maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupona na nilitaka kufanya misa maalumu ya kuwakumbuka marehemu wakiwamo baba na mama yangu.”

Alisema kusambaa kwa taarifa hiyo kulisababisha simanzi kwa ndugu, jamaa na watoto wake wanaoishi ndani na nje ya nchi jambo ambalo lilisababisha watu kutoa vilio.

Mrema ambaye aliwahi kuwa naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani ya nchi, aliliomba Jeshi la Polisi lichunguze haraka ili mtuhumiwa huyo apatikane na kufunguliwa mashtaka.

Mbali ya sababu hizo, Mrema alidai kwamba kusambazwa kwa ujumbe huo ulikuwa ni mpango wa wanasiasa kuwapoteza wananchi wasimfuatilie Rais John Magufuli alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa Ikulu na badala yake wafuatilie kifo chake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema suala hilo la Mrema linalishughulikia kwa taratibu za jeshi hilo na watakaobainika watachukuliwa hatua.