In Summary

Kamwelwe amesema mradi usipokamilika hadi Februari mwakani atafuta mkataba.

Chalinze. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe ametishia kuufuta mkataba wa utekelezaji mradi wa maji wa Wami Chalinze kutokana na kasi ya ujenzi kutoridhisha.

Kamwelwe ametoa tishio hilo jana Jumatano Desemba 6,2017, Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alikotembelea mradi wa maji kujionea maendeleo ya ujenzi. Amesema ifikapo Februari 8, mwakani kama mradi hautakuwa umekamilika mkataba utafutwa.

Katika ziara hiyo waziri alifuatana na mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete; Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga; mwenyekiti wa halmashauri na wataalamu.

"Si bure, mbunge Ridhiwani Kikwete umekuwa ukipiga kelele kuhusu kusuasua mradi huu, leo nimejionea mwenyewe uhalisia na sasa kama Serikali tunakwenda kuangalia namna ya kuvunja mkataba," amesema.

Mradi huo ulikuwa ukamilike Februari lakini baada ya majadiliano ilikubaliwa ukamilike Oktoba na hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Ridhiwani ameishukuru Serikali kwa hatua ilizochukua kimkataba na kumkumbusha waziri kuwa mradi huo ni wa muda mrefu lakini hakuna dalili za maji kupatikana Chalinze.

"Kazi inakwenda taratibu, hakuna dalili ya wana Chalinze kunywa maji safi na salama mapema mwakani," amesema Ridhiwani.

Amemuomba waziri azidishe kasi ya usimamizi ili kabla ya kipindi cha pili cha mwaka 2018 kazi iwe imekwisha.

Awamu ya tatu ya mradi wa Wami Chalinze inatekelezwa na mkandarasi Overseas Infrastracture Alliance (OIA) PV Ltd ya nchini India.

Mradi huo ukikamilika utahudumia wakazi 234,394 wa jimbo hilo.