In Summary

Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu  Irenius Ruyobya amesema kupungua kwa mfumuko wa bei  Oktoba,  kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.

Dar es Salaam. Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa Oktoba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 5.3 ilivyokuwa Septemba, 2017.

Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia  Oktoba, 2017 imepungua  ikilinganishwa na  Septemba, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu  Irenius Ruyobya amesema kupungua kwa mfumuko wa bei  Oktoba,  kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.

“ Kupungua kwa mfumuko wa bei Oktoba kumechangiwa na kushuka kwa gharama za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Oktoba, zikilinganishwa na bei za Oktoba, mwaka jana ‘’,amesema  Ruyobya.

Ametaja  baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kuwa ni pamoja na unga wa mtama umepungua kwa asilimia 2.6, samaki kwa asilimia 7.1, matunda kwa asilimia 2.7, mbogamboga kwa asilimia 7.4,maharage kwa asilimia 2.9, viazi kwa asilimia 14.4 na karanga kwa asilimia 7.8.

Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.