In Summary

Kayombo amesema tatizo hilo lilitatuliwa jana lakini leo asubuhi lilijirudia.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema mfumo wa forodha (Tancis) umepata hitilafu.

Katika taarifa ya mamlaka hiyo kwa umma imesema hitilafu hiyo ambayo haikukusudiwa na hasa katika kiunganisho kati ya TRA na mawakala wa forodha imesababisha kadhia za mizigo kushindwa kushughulikiwa.

Richard Kayombo, mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi, TRA katika taarifa hiyo ya leo Alhamisi Desemba 7,2017 amesema jana walitatua tatizo hilo lakini leo asubuhi lilijirudia.

“Wataalamu wa mifumo hivi sasa wanafuatilia kwa makini kutambua chanzo cha hitilafu hii kujirudia ili kupata ufumbuzi wa kudumu,” amesema.

Kayombo amesema kuna dalili njema, hivyo amewaomba wadau wawe na subira na kwa wakati huohuo amewaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.

Amesema usumbufu huo si tu unaathiri shughuli zao bali hata ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Wadau hao ni waagizaji na wasafirishaji wa mizigo nje ya nchi na wananchi kwa jumla.

“Mamlaka itaendelea kutoa taarifa kwa kadri tatizo hili linavyoshughulikiwa na pindi ufumbuzi utakapopatikana mtajulishwa,” amesema.