In Summary

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema siri ya mshikamano wa viongozi wa chama hicho ni kufanya kazi kama watu wa familia moja bila ya kujali nafasi zao za uongozi.

 

Morogoro. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema siri ya mshikamano wa viongozi wa chama hicho ni kufanya kazi kama watu wa familia moja bila ya kujali nafasi zao za uongozi.

Mbowe amesema hayo leo Jumamosi mara baada ya ibada ya mazishi ya mama mzazi wa wakili maarufu wa kujitegemea Peter Kibatala, Anastazia Mayunga iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Maria Consolata Parokia ya Sua.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Mbunge wa Morogoro Mjini(CCM), AbdulAziz Abood na wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi, John Mnyika, Godbless Lema, Suzan Kiwanga na Devotha Minja.

Amesema Chadema imeguswa na msiba wa mama wa wakili huyo ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akikisaidia chama katika kutetea kesi mbalimbali zinazowakabili viongozi na wanachama wa Chadema na ndio maana waombolezaji wengi waliohudhuria msiba huo ni kutoka Chadema .

Mwenyekiti huyo amesema kwa kutambua umuhimu wa wakili Kibatala chama kimeamua kuhairisha kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho ambayo ilipaswa kuketi leo Jumamosi ili kutoa fursa kwa viongozi wake wakuu kuhudhuria mazishi ya mama mzazi wa wakili huyo aliyefariki baada ya kuangukiwa na ukuta.