In Summary
  • Asema Watanzania wanataka mabadiliko ya kweli na ya kudumu
  • Akizungumza katika mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Chanikanguo katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara juzi, Mbowe aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa Watanzania wengi wameelimika na wanataka mabadiliko ya kweli na ya kudumu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepiga ‘siasa za urais’ kwenye kampeni za marudio ya udiwani baada ya kuwataka watu wanaohitaji mabadiliko kukipa nafasi chama hicho kwa miaka mitano.

Akizungumza katika mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Chanikanguo katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara juzi, Mbowe aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa Watanzania wengi wameelimika na wanataka mabadiliko ya kweli na ya kudumu.

“Sisi shida yetu siyo, unachagua chama gani bali chama unachokichagua kitakufanyia nini katika kuleta maendeleo. Tumepewa fursa ya kujisahihisha tuitumie ipasavyo kwa kuchagua viongozi wanaoona mbali na wenye fikra za mafanikio kwa wote,” alisema Mbowe.

Alisema kila siku kunahubiriwa maendeleo, lakini kiuhalisia hayapo ikiwamo wakulima wa korosho kunufaika kwa asilimia 20 kutokana na kile wanachokifanya huku asilimia 80 ikinufaisha nchi za nje. 

“Sisi tunaunga mkono sera ya viwanda, lakini tunataka iwanufaishe wakulima. Kuwe na viwanda vya kuiongezea zao thamani,” alisema.

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe alisema wamevuna wanachama 300 kutoka CCM ndani ya wiki mbili tangu kuanza kampeni za udiwani, hivyo hiyo inaonyesha kuwa kuna vitu wananchi wanakosa, hasa kutokana na zuio la kutofanya mikutano ya siasa.

“Wiki mbili tu tumefanikiwa kuvuna idadi hiyo ya wanachama, siasa zingekuwa zinaendelea kama kawaida wengi wangehama kutokana na kuelewa nchi inakwenda wapi na inahitaji nini ili kusonga mbele kwa amani na haki.

“Kura 1,600 tulizikosa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015 ambao wanachama wa CCM ndiyo walitukosesha kura hizi, lakini leo hii tumefanikiwa kuvuna idadi hii ya wanachama wa CCM ndani ya wiki mbili katika kata ya Chanikanguo,” alisema Mwambe.