Dar es Salaam. Dk Louis Shika, mteja aliyejitokeza kununua nyumba za mfanyabiashara mashuhuri nchini, Said Lugumi, amejikuta akitupwa rumande baada ya kuzua utata wa malipo ya awali na kutoa majibu yanayojikanganya.

Mnada huo ambao ulifanyika jana katika nyumba za Lugumi zilizopo Mbweni JKT na Upanda uliendeshwa na kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufidia Sh14 bilioni za kodi ambazo Lugumi anadaiwa. Dk Shika akifikia bei ya kuzinunua zote kwa Sh3.2 bilioni.

Utata uliibua pale alipotakiwa kulipa asilimia 25 ya gharama ya kila nyumba kama sheria ya mnada inavyotaka. Nyumba ya kwanza alifika bei ya Sh900 milioni ya pili Sh1.1 bilioni zote za Mbweni JKT huku ile ya Upanga akifikia bei ya Sh1.2 bilioni. Baada ya kushindwa kulipa, alipelekwa Kituo cha Polisi Selander ambako aliomba kompyuta mpakato ili afanye muamala kutoka nje ya nchi kwenda akaunti ya TRA, ambao alisema ungechukua dakika tano. Hata hivyo, ilishindikana na kusema inahitaji saa 48.

Hatua hiyo iliwafanya Yono na mmoja wa maofisa wa TRA kujadiliana na ofisa wa TRA alisikika akisema “Haiwezekani, huyu anahitaji kupelekwa Central (Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda ya Dar es Salaam) na Kamishna amesema huyu asiachiwe.”

Kabla ya safari ya kwenda Central, Dk Shika alimweleza mwandishi wetu ambaye alikuwapo eneo hilo kwamba, “Watu wanasemasema huko mitandaoni, nitawazima midomo nikilipa, subirini mtaona labda hawa wakatae kwani ndani ya saa 48 zitakuwa zimewasili, fedha kidogo sana hizo bilioni tatu kidogo sana.”

Utata wa suala hilo ulianza baada ya mnada kumalizika na maofisa wa TRA kumchukua kwenda benki kwa kufanya malipo ya asilimia 25 ya Sh3.2 bilioni ambazo ni Sh700 milioni ndipo alipowaeleza kuwa hana fedha mkononi au benki hadi afanye muamala kutoka nje ya nchi.

“Sheria ya mnada ni lazima alipe asilimia 25 siku hiyohiyo na sisi tulitangaza matangazo, sasa anaposema hana fedha na anajua kabisa anatakiwa kulipa asilimia 25 hatumwelewi, katuharibia mnada wetu na itabidi urudiwe kwa nyumba mbili,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela baada ya kuelezwa Dk Shika ameshindwa kulipa.

Kevela alisema nyumba ya Mbweni JKT ambayo Dk Shika alifikia bei ya Sh1.1 bilioni ilichukuliwa na Justo Malika kwa Sh.1 bilioni na nyumba zingine mbili mnada utarudiwa huku Malika akisema, “Nashukuru nimeinunua nyumba hii, kwani naitaka sana kwa makazi ya familia yangu.’’

Dk Shika alianza kuzua minong’ono mara baada ya kuibuka mshindi kwa nyumba ya kwanza ya Sh900 milioni hasa kutokana na usafiri alioutumia kufika pale, mwonekano wake kimavazi na kushindwa kujibu maswali ya msingi aliyoulizwa na mwandishi wetu.

Miongoni mwa maswali hayo ni umri wake. Awali alisema haujui na alipoonyeshwa pasi yake ya kusafiria ambayo inaonyesha kuwa alizaliwa Desemba 31, 1969 huko Nyegezi, Mwanza alijibu, “Huo ni umri tu ambao niliutumia kupata pasipoti, umri wangu siukumbuki nilizaliwa zamani.’’ Alipoulizwa makazi yake alisema anaishi Tabata Mawenzi na Kigamboni lakini katika mahojiano aliyofanyiwa katika Kituo cha Selander alisema anakaa Tabata Mawenzi na hakuitaja Kigamboni.

Awali, mwandishi wetu alimuuliza ana watoto wangapi na familia yake ipo wapi na alijibu, “Iko Marekani na watoto mimi sijui. Unajua anayejua una watoto wangapi ni mama yao, hata wewe (mwandishi) unaweza kukuta baba yako si yeye, lakini Marekani ninao wawili na nchini Urusi ninao wawili.”

Alipoulizwa alikopata fedha za kununua nyumba hizo alisema, ‘‘Mimi ni daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu, Rais wa kampuni ya kimataifa ya Ralcefort ya nchini Urusi, inayojishughulisha kemikali za viwandani na pia ni Balozi wa UNHCR. Hivi vyote ni vyanzo vyangu vya mapato hasa hii kampuni.”

Lakini licha ya kudai kwamba ina matawi Ujerumani, Kenya na Hispania, mwandishi wetu hakufanikiwa kuiona kampuni hiyo kwenye mitandao.