Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha amerejea CCM baada ya kujiondoa Chadema alichokitumikia kwa miaka miwili.

Masha alitoa taarifa yake jana jioni huku akidai upinzani wa sasa umeridhika na hali ya kuendelea kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama tawala kujirekebisha.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini hauna nia wala sababu ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia falsafa, sera na uongozi mbadala.” Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuwa waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Awamu Nne, alisema upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea udhaifu wa CCM badala ya uwezo wake kama mbadala.

Alisema kazi ya chama cha siasa ni kujiandaa na hatimaye kushinda uchaguzi ili kiweze kuunda na kuendesha Serikali na dola kama njia ya maono yaliyo kwenye ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuleta maendeleo na ustawi.

“Nilijivua uanachama CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema nikiamini nitashiriki kukifanya chama hiki kikomae na kufikia hatua ya kuwa mbadala kifalsafa, kisera na uongozi,” alisema.

Hata hivyo, uzoefu wangu wa miaka miwili ndani ya Chadema umenionyesha chama hiki kina safari ndefu kisiasa na kuwa chama mbadala cha kuunda Serikali.” alisema.

“Mpaka sasa chama hiki kimeendelea kujikita katika kukosoa na kuonyesha udhaifu wa Serikali hasa Rais John Magufuli binafsi. Natambua kwamba kukosoa ni kazi muhimu ya chama cha upinzani, kazi hii haikifanyi chama kuwa mbadala cha kuunda Serikali.”

Masha ambaye pia aliwani kuwa mbunge wa Nyamagama kati ya 2005-2010 na baadaye kushindwa, alisema si sahihi kwa vyama vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Rais Magufuli ambaye ni mkuu wa nchi pekee anayetekeleza kwa vitendo mambo ambayo upinzani ulikuwa ukiyapigia kelele kwa miaka mingi na kuwashinda viongozi wa CCM waliomtangulia. “Nimejivua uanachama kuanzia leo (jana), nina imani uamuzi huu utanipa fursa ya kutafakari kwa kina safari yangu ya kisiasa ndani ya nchi hii. Nawashukuru viongozi wa Chadema kwa miaka miwili ya kufanya kazi pamoja nao, nawatakiwa kila la heri,” alisema mwanasiasa huyo ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioshiriki kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumzia uamuzi wa Masha, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema wao wanapokea ushauri wa kukoselewa na mwanachama yeyote kwa kuwa ni haki yao, lakini kwa sababu alizozitoa Masha si za msingi.

“Miaka miwili aliyokaa alikuta chama kina sera, itikadi hivyo aseme nini ambacho anakwenda kufanya,” alisema Dk Mashinji.