In Summary

Uzinduzi huo unafanyika katika stesheni ya Ihumwa mkoani Dodoma


Dodoma. Shirika Hodhi la Raslimali za Reli (Rahco) limetoa usafiri wa treni kwa ajili ya kuwapeleka wakazi wa Dodoma katika eneo la uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambao unafanywa na Rais Dk John Magufuli asubuhi hii Machi 14, 2018.

Mapema asubuhi, wakazi hao wamekusanyika katika stesheni ya reli ya Dodoma kwa ajili ya kusubiri usafiri huo, mabehewa sita yalikwenda mara mbili kuwapeleka watu eneo unakofanyika uzinduzi huo katika stesheni ya Ihumwa mjini hapa.

Kufuatia usafiri huo, idadi ya kubwa ya wananchi walijitokeza kushuhudia uzinduzi huo kutoka Morogoro hadi Makutopora mkoani hapa.

Treni ya kwanza iliondoka saa 1:20 asubuhi kuwapeleka watu eneo la Ihumwa na ya pili iliondoka saa 2:46 asubuhi huku watu wengi wakiwa wamesimama.

Katika maeneo mengine iliposimama treni hiyo kwa lengo la kuchukua watu wanaokwenda katika uzinduzi huo, ilishindwa kuwachukua kutokana na kujaa kwa mabehewa hayo.

Hata hivyo, baadhi ya abiria waliuokuwa na shauku ya kuutumia usafiri huo walikwenda na treni ya kwanza na kurejea nayo tena mjini kabla ya kurudi tena Ihumwa kwa ajili ya uzinduzi huo.

“Mimi sijawahi kupanda treni hata siku moja, kumbe iko hivi nashukuru sana,” amesema Mwanaisha Isasa mkazi wa Chang’ombe mjini Dodoma.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na wabunge na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Rahco, Masanja Kadogosa amesema mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Morogoro na Dodoma ulisainiwa Septemba 29, mwaka jana kati ya Kampuni ya Rahco na Yapi Merkezi Inssar Sanay’s ya Uturuki.

Treni hiyo ya mwendokasi itakuwa ikisafiri umbali wa kilomita 160 kwa saa itajengwa kwa gharama ya dola 3.457 za Marekani.