Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashta katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili  Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake, kukamilisha upelelezi.

Hakimu Mkazi Mkuu,Wilbard Mashauri akitoa wito huo leo Ijumaa kwa upande wa mashtaka mara baada ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Baada ya kutolewa maelazo hayo,  wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko aliomba  upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa kuwa inaonekana umekamilika lakini  upande wa mashtaka unachelewesha.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24 , 2017  kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga.

Wanakabiliwa na mashtaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha kwa  Dola za Marekani, 375,418.