In Summary
  • Pia amewataka viongozi hao kuacha urasimu kwa wananchi na kufikiria maenedeleo

Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza viongozi wa halmashauri na majiji nchini kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi na kuachana na urasimu unaosababisha kuwepo kwa ujenzi holela .

Lukuvi ameyasema  hayo alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa nyumba  kumi za  mfano za mradi wa mji wa kisasa wa  Safari City  zilizopo eneo la Mateves sambamba  na kutoa hati miliki kwa wanunuzi 100 wa kwanza wa viwanja zinazotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Amesema kuwa kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe na hivyo kuchangia  wananchi hao kujenga kiholela kutokana na kuchoka kusubiri  kwa muda mrefu. 

Aidha kufuatia hali hiyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kufanya ukaguzi wa mafaili ya vibali vya ujenzi na kuweza kugundua idadi ya watu ambao hawajapatiwa vibali vyao mpaka sasa hivi.

"Unajua idadi kubwa ya wananchi wanaojenga kiholela siyo kwamba wamevunja sheria bali wanafanya hivyo kwa ajili ya ucheleweshaji wa vibali  na msiwalazimishe wananchi kusubiri kwa muda mrefu sana bila kuwapatia majibu yanayoeleweka kwani nyie wenyewe ndio mtakuwa mnachangia ujenzi holela. "amesema Lukuvi. 

Lukuvi amesema kuwa, ni aibu na fedheha wananchi kukaa katika maeneo holela kwani wanachangia kuharibu madhari ya Jiji ,na hivyo kuwataka kujenga maeneo yaliyopimwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nyumba la taifa Nehemia Mchechu amesema kuwa mradi huo wa kitovu cha mji wa kisasa wa safari city jijini hapa una ukubwa wa hekari 559.4 na ni sehemu ya miji iliyopangiliwa kitaalamu na kwa kuzingatia sheria za mipango miji.

"Mradi huu ulibuniwa na shirika la nyumba kwa lengo la kupunguza uhaba wa makazi kwenye jiji hili ambapo tumetenga maeneo kwa ajili ya waendelezaji kujenga sehemu za biashara,burudani ,utalii,hospitali, elimu,huduma za kijamii kama vile polisi,na zimamoto lakini pia yapo maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo na mapumziko"amesema Msechu.