In Summary

Kiini cha kadhia hiyo ni hatua ya mbunge huyo kukituhumu kiti kuwa kilisema alipewa 'vidonge' na Waziri wa Afya.

 

 

Dodoma.  Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga hasa aliposema yeye sio mbunge wa kuteuliwa na mtu mmoja, ulionekana kumkera Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Kiini cha kadhia hiyo ni hatua ya mbunge huyo kukituhumu kiti kuwa kilisema yeye (Mbunge), alipewa vidonge na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akijibu hoja za wabunge jana Jumatatu jioni.

Dk Tulia alienda mbali na kueleza kuwa hata wabunge wa kuteuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba ya nchi, nao wamepigiwa kura na nchi nzima kwa sababu aliyewateua anazo kura za nchi nzima.

“Susan Kiwanga ametumia maneno ambayo kwa kweli yeye anajua alipoyatoa. Sina uhakika kama aliyatoa kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge) hata ya jana au leo,” alisema Naibu Spika.

“Maneno ya vidonge vya mtu hapa si maneno ya kibunge. Hiki kiti hakijasema hayo maneno. Kiti kimesema ulipewa majibu wala si vidonge. Vidonge sio lugha ya kiti hiki wala lugha ya kibunge”.

Naibu Spika alisema Waziri Ummy alikuwa anachangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 kama Mbunge mwingine yoyote kama Susan naye alivyochangia.

“Mheshimiwa Mpango ameleta Mpango ukachangia na yeye akaamua kuchangia vile alivyoona inafaa. Mimi nilikukumbusha tu kuwa ulipewa majibu ya ziada sijasema ulipewa vidonge,” alisema Dk Tulia.

“Jambo moja la msingi ambalo tumelisisitiza sana ni kwamba wabunge wakishafika humu kiapo ni cha aina moja. Mtu asifike mahali akamdharau Mbunge mwenzie kwa sababu yoyote ile,” alisema.

“Nilishawahi kutoa ufafanuzi mahali pengine kwa sababu wabunge wa viti maalum sina hakika na wa vyama vingine lakini wabunge wa viti maalum wa CCM wanapigiwa kura kwenye mikoa,” alisisitiza.

“Sasa ni vizuri waheshimiwa wabunge tukayafahamu mambo haya na tutoe heshima kwa kila mtu inayotakiwa,” alisema Naibu Spika ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais na akaongeza kusema;-

“Mheshimiwa Susan Kiwanga umezungumzia wabunge wa kuteuliwa ambao kikatiba wako 10 na wale wanateuliwa na mtu ambaye amepigiwa kura nchi nzima,”.

“Kwa hivyo, hata wabunge wa viti maalum wanapigiwa kura , wabunge wa kuteuliwa wao wamepigiwa kura na nchi nzima kwa sababu aliyewateua anazo kura za nchi nzima”.

“Kwa hiyo lazima kila mtu apewe heshima anayostahili. Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya) alikuwa akichangia kama wabunge wengine,” alisisitiza Naibu Spika.

Akiomba mwongozo wa kiti, Mbunge huyo, alisema Naibu Spika alimweleza kuwa juzi alipewa vidonge vyake kutokana na mchango wake bungeni juzi lakini hakuwepo bungeni.

Alisema wakati Waziri akitoa majibu hayo, yeye alikuwapo viunga vya Bunge akizungumza na wapiga kura wake na kwamba aliyekuwa akimpa vidonge ni Mbunge wa Viti Maalum.

“Ninapokuwa natoa maelezo yangu kuhusu mpango, nakuja napewa vidonge. Vidonge sikupewa mimi wamepewa wananchi wa Jimbo la Mlimba. Mimi ni Mbunge wa Mlimba wala sikuteuliwa”.

“Sasa tunapokuja hapa tunakuja kama mwakilishi wa wananchi waliopiga kura. Sikuteuliwa mimi na mtu mmoja mheshimiwa Naibu Spika,” alisema Susan na kuongeza kusema kuwa;-

“Kwa hiyo naomba mwongozo wako ni namna gani mimi Mbunge ninaweza kuchangia mpango halafu Waziri sijamtaja anakuja ananipa vidonge. Sijui vidonge gani Panadol au Quinnine”.

Wakati Naibu Spika alitoa mwongozo huo, wabunge walio wengi wa CCM walionekana kufurahishwa na maelezo hayo huku mara kwa mara wakipiga meza kuonyesha kumuunga mkono Dk Tulia.