In Summary

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraji Mnyepe imesema Rais Magufuli ametengua uteuzi wa balozi wa Tanzania nchini Canada, Alphayo Kidata.

Dar es Salaam. Januari mwaka huu, Alphayo Kidata alibeba habari kubwa ya gazeti hili lilipomtaja kwamba anaweza kuwa mtu pekee katika Serikali ya Awamu ya Tano ambaye ameshika zaidi ya nafasi tatu muhimu katika miaka miwili.

Kidata alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; akateuliwa kuwa kaimu kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kabla ya kuthibitishwa kuwa kamishna kamili.

Katika nafasi hiyo hakudumu muda mrefu akateuliwa kuwa katibu mkuu (Ikulu) ambako nako hakukaa kipindi kirefu akateuliwa kuwa balozi na kupangiwa nchini Canada, ikiwa ni nafasi ya nne kubwa kuishika tangu 2015.

Lakini jana, taarifa ya aya moja iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilikuja na habari mbaya dhidi ya Kidata, ikisema Rais John Magufuli ametengua uteuzi na kumrejesha nchini.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo ilichukuliwa tangu Jumatatu iliyopita, imekwenda sambamba na kumvua hadhi ya ubalozi.

Taarifa hiyo iliyotolewa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Faraji Mnyepe haikufafanua zaidi.

Machi 2016, Rais Magufuli alimteua Kidata kuwa kaimu kamishna mkuu TRA na baadaye kumthibitisha kuwa kamishna mkuu.

Kabla ya uteuzi huo, Kidata alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nafasi aliyoishikilia tangu Agosti, 2013 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) ambako alikuwa naibu katibu mkuu.

Machi 23, 2017 aliteuliwa kuwa katibu mkuu (Ikulu) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Peter Ilomo ambaye alistaafu. Alidumu katika nafasi hiyo tangu wakati huo hadi Januari 10 alipoteuliwa kuwa balozi.

Uteuzi wa Kidata kuongoza TRA ulitokana na mshikemshike ulioibuka katika mamlaka hiyo baada ya Novemba 27, 2015, Rais Magufuli kumsimamisha kazi aliyekuwa kamishna mkuu, Rished Bade baada ya kuibuliwa kwa upotevu wa makontena 249 yenye thamani ya Sh80 bilioni katika Bandari ya Dar es Salaam pasipo TRA kuwa na kumbukumbu zozote.

Katika mabadiliko hayo, Rais alimteua Dk Philip Mpango kukaimu nafasi hiyo, lakini Desemba 23, 2015, alimteua kuwa mbunge na kisha Waziri wa Fedha na Mipango, na Kidata kukaimu nafasi hiyo.