Arusha. Serikali imepinga hoja zilizowasilishwa kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) na mashirika matatu yanayodai Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016 inakiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na inaminya uhuru wa habari.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mark Mulwambo akisaidiwa na Sylivia Matiku mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Monica Mugenyi, Fakihi Jundu na Dk Faustin Ntezilyayo alisema hoja hizo hazina msingi na kuiomba Mahakama izitupilie mbali.

Hata hivyo Jaji Mugenyi alizitaka pande mbili kukutana kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye hati zilizowasilishwa mahakamani kwa ajili ya kuandaa hati kamili ya kuanza kusikilizwa rasmi kwa kesi hiyo.

Kesi hiyo imefunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Shirikisho la Watetezi wa Haki za Binadamu(THRDC) wakipinga sheria ya huduma ya vyombo vya habari sura namba 12 ya 2016 iliyopitishwa na Bunge Novemba 5, 2016.

Katika maombi yao wanadai kuwa sheria hiyo inakiuka itifaki iliyoanzisha EAC kwenye ibara 6(c) na 7(2) ambayo Tanzania ni mwanachama na inapaswa kulinda na kuiheshimu ikiwa ni nchi mwanachama.

“Serikali ya Tanzania imeshindwa kuheshimu na kutekeleza masharti ya vifungu 6(d) na 7(2) ya mkataba wa Afrika Mashariki vinavyotaka kuheshimu na kuinua haki za binadamu sanjari na kuzitambua haki,” inaeleza sehemu ya maombi hayo. Jaji Mugenyi ametoa mwezi mmoja hadi Aprili 13 mwaka huu walalamikaji wawasilishe hati za viapo na marekebisho ya hoja huku upande wa Jamhuri ukitakiwa uwe umejibu hoja hizo na kuziwasilisha katika mahakama hiyo kabla ya Mei 14.