In Summary

Viongozi wa mitaa walonga

Dar es Salaam. Kutakiwa kuhamishwa kwa madalali wa magari katika maeneo yao wanayofanyia kazi jijini Dar es Salaam kumeelezwa kuwa huenda kukaibua wimbi jipya la vijana kujihusisha na matukio ya uhalifu.

Kauli hiyo imekuja baada ya kiongozi mmoja mkoani Dar es Salaam kuliagiza Jeshi la Polisi kuwasambaratisha wafanyabiashara wa magari (Madalali) wanaoyauza katika maeneo yasiyo rasmi na kuisababishia serikali kukosa mapato.

Kiongozi huyo alitoa agizo hilo hivi karibuni jijini humo huku akitaka wajiunge na wenye leseni kubwa kusudi wakatwe kodi.

Kauli hiyo imepingwa kwa madai kuwa wauza magari hao hawana mitaji ya kutosha ndiyo maana wanauza mitaani bila kufanya vurugu wala kumdhuru mtu.

Mmoja wa madalali hao, Evans Komu alisema wanapenda kuwa na ofisi maalumu kwa sababu itawaongezea uaminifu pia kwa wateja wao, lakini mitaji yao bado midogo.

Alisema kwa sababu wanafanya biashara kwenye mitaa na wanatambulika, ipo njia rahisi ya wao kubanwa na kulipa kodi kupitia wenyeviti wa Serikali za mitaa.

Dalali mwingine anayefanya shughuli zake eneo la Ilala, Shukuru Ismail alisema hali ya uchumi ni ngumu na ajira hakuna, wao wamejaribu kufanya biashara hiyo lakini bado baadhi ya viongozi wanawaona kuwa ni wahuni.

Hata hivyo, Diwani wa Mzimuni, Ally Kondo alisema hapingi kuondolewa wafanyabiashara hao kwa kigezo cha kulipa kodi, anachotaka kufahamu watapelekwa wapi.

Alisema wengi wao bado wana mitaji midogo, kuungana na wenye mitaji mikubwa hawatapata faida.

Aliomba kauli ya kiongozi huyo iangalie namna nzuri ya kuwasaidia badala ya kuwafukuza.

Bakari Kasubi, Diwani wa Mtambani alisema kauli ya kuwatimua si sahihi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inahangaika kuwatafutia ajira vijana. “Inaweza pia kusababisha mrundikano wa magari kwenye yadi, hapa Mtambani kuna eneo moja la kijiwe cha madalali lakini bado kuna mrundikano wa magari. Serikali ya mkoa ifanye utafiti wa kina kabla ya kuendelea na hatua hiyo,” alisema.

Alishauri badala ya kuwatimua, itafutwe njia mbadala itakayowafanya walipe kodi kama ilivyo kwa wachimbaji wadogo wa madini.

Kauli ya Kasubi iliungwa mkono na Ally Bachu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dosi, Magomeni aliyesema: “Kama mtu hujamtafutia mchumba usimwambie amuache mkewe, kwa sababu atazini, hivyo kabla ya kuwafukuza wawatafutie maeneo ya kufanya shughuli zao.”