In Summary

HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ikiwa na jukumu la kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa Watanzania wahitaji na wenye sifa.


Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwezi ujao itaanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/19.

Upokeaji maombi utaanza Mei, 2018 baada ya kukamilisha uboreshaji wa mfumo wa uombaji kwa njia ya mtandao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa aliyoitoa leo Jumanne, Aprili 17, 2018, amesema maombi yote yatapokewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umeboreshwa na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).

Badru amesema pia watatangaza mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa kuwasilisha maombi; tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi; sifa na vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa masomo unaotarajiwa kuanza Oktoba, 2018. 

“Tunawasihi wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa Mei, 2018 na kuuzingatia,” amesema Badru.

Amesema mwaka jana zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vile vyeti vya kuzaliwa au hata vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kama ilivyoelekezwa. 

Nyaraka nyingine ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne; cha sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na kamishna wa viapo yaani wakili au hakimu.

Badru amesema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa mganga mkuu wa mkoa, wilaya au kituo cha afya cha Serikali.

Amesema wanafunzi waliofadhiliwa katika masomo ya sekondari au stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka taasisi zilizogharamia masomo yao.

Badru amesema maofisa wa HESLB watatembelea mikoani kukutana na waombaji wa mikopo kuwaelimisha kuhusu utaratibu sahihi wa kuwasilisha maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao.