In Summary

Watoto wawili wa dos Santos, waliokuwa wamepewa majukumu makubwa wakati wa utawala wa baba yao hivi sasa wanachunguzwa kwa ufisadi.

 


Luanda, Angola. Viwanja vya Independence Square katikati ya jiji la Luanda vilipokea makundi mawili ya waandamanaji yote yakiwa na uhusiano wa namna fulani na rais wa zamani, Jose Eduardo dos Santos.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari na mtafiti wa haki za binadamu, Zenaida Machado, hiyo ilikuwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kwamba wanaharakati waliweza kufanya maandamano bila kudhibitiwa na polisi.

“Hakukuwa na mbwa, farasi, wala bakora… Hongera Polisi wa Angola. Endeleeni vivyo hivyo,” aliongeza mwanamama huyo katika ujumbe wake wa Twiter Jumapili. Baadaye alifafanua kwamba picha zilizokuwa zimeambatana na tweet zake zilihusu makundi mawili ya waandamanaji.

“Kwa ufafanuzi: matukio mawili yalifanyika hapo. Moja lilikuwa la waendesha pikipiki ambalo liliandamana kumuunga mkono Dos Santos, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani. Na la pili, ambalo ni muhimu sana kwangu, wanaharakati wakiwemo wafuasi wa kundi la 15+2 wakitoa wito Dos Santos “rudisha fedha,” alisema.

Eduardo dos Santos ameongoza Angola kwa karibu miongo mine kabla ya kujiuzulu mwaka 2017 kabla ya uchaguzi mkuu. Chama tawala cha MPLA kilimteua aliyekuwa waziri wa ulinzi Joao Lourenco kuwani urais na alishinda kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura.

Lourenco aliyeahidi kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya uchumi amechukua hatua kali zilizoongozwa na taasisi ya kupambana na ufisadi.

Watoto wawili wa dos Santos, waliokuwa wamepewa majukumu makubwa wakati wa utawala wa baba yao hivi sasa wanachunguzwa kwa ufisadi. Isabel aliongoza shirika la mafuta la Sonangol wakati kaka yake Filomeno aliongoza mfuko wa wakfu wa Angola, ambapo sasa yote yako chini ya ofisi ya rais.